‘Tuliondoka kwa machela, tumerudi tukitembea’

WATOTO watatu wa Shule ya Msingi ya Lucky Vicent ya jijini Arusha waliopelekwa nchini Marekani kutibiwa baada ya kupata ajali wamerejea nchini na kusema wanamshukuru Mungu kwa vile waliondoka wakiwa katika machela na sasa wamerejea wakiwa wanatembea wenyewe.

Hafla ya kuwapokea watoto hao Doreen Mshana, Wilson Tarimo na Sadya Awadhi ilifanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wanafunzi wenzao wa Shule ya Kimataifa ya Lucky Vicent na wanafunzi wa shule nyingine, huku tukio hilo likigubikwa na hisia za furaha iliyochanganyikana na hudhuni kutokana na kukumbusha tukio la ajali yenyewe.

Katika ajali hiyo, wanafunzi 32 wa darasa la saba, walimu wawili na dereva wa gari la shule hiyo walipoteza maisha katika eneo la Rhotia, Marera wilayani Karatu mkoani Arusha, Mei 6 mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika tukio hilo akimwakilisha Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye yupo nchini Afrika Kusini akimwakilisha Rais John Magufuli kwenye Mkutano wa Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Wakizungumza mara baada ya kuwasili uwanjani hapo watoto hao walitoa shukrani kwa serikali na makundi mbalimbali wakiwemo viongozi, madaktari, wauguzi na Watanzania wote kwa mchango uliofanikisha wao kurejea wakiwa na afya njema.

Akizungumza katika mapokezi hayo, Wilson aliishukuru serikali ya Tanzania kwa kuwezesha safari yao ya kwenda Marekani kwa matibabu kuwa ya ufanisi na mafanikio makubwa mara baada ya watoto hao kupewa fursa ya kila mmoja kutoa neno ya shukrani mbele ya Mkuu wa Mkoa, Mghwira.

“Tunaishukuru serikali ya Tanzania kwa kutusaidia kupata hati za kusafiria sisi na wazazi wetu, lakini pia daktari na muuguzi ambao tulisafiri nao. Sina mengi ya kusema ila nawashukuru kwa sala na dua zenu kwani tuliondoka tukiwa kwenye machela na leo tumerejea tukiwa tunatembea wenyewe,” alisema Wilson na kuamsha simanzi yenye mchanganyiko na furaha kwa walioshuhudia mapokezi hayo.

Naye mtoto Doreen alisema: “ Nawashukuru wote kwa maombi yenu maana hali yangu ilikuwa mbaya kuliko wenzangu, naomba muendelee kuniombea. “Nawashukuru madaktari wa Tanzania na Marekani wamenisaidia sana maana sikuwa na fahamu kwenye viungo vya mwili wangu lakini leo hii ni mzima, naomba muendelee kuniombea”.

Sadya kwa upande wake alisema hana neno la shukrani zuri zaidi ya asante na kwamba Mungu ni mweza wa yote kwani amefanya mema katika maisha yake na aliwashukuru madaktari waliowasaidia hadi kurejea wakiwa salama.

Naye mzazi wa Doreen, Neema Elibariki alisema: “ Tunamshukuru Mungu kwa kurudi salama huku watoto wetu wakiwa wazima” Akizungumza katika tukio hilo, Mghwira aliwashukuru madaktari wa Marekani na serikali yao akisema mbali ya kuwarudhisha salama watoto hao, wameleta vifaa vya kusaidia hospitali mbalimbali.

Pia alikabidhi hati maalumu ya utambuzi wa mchango wa kuokoa maisha ya hao watoto hao kwa Mbunge wa Singida, Lazaro Nyalando, Steve King ambaye ni Mjumbe wa Bunge la Marekani na Dk Steve Meyer ambaye ni daktari bingwa wa mifupa aliyeongoza jopo la madaktari waliowatibu watoto hao na Mkurugenzi Mwenza wa Shirika la Stem linalodhaminiwa na Samaritan’s Pass.. Naye Nyalandu aliyefanya kazi kubwa ya uratibu wa matibabu ya watoto hao alisema ni furaha kuona watoto hao wamerejea wakiwa wazima.

Alimshukuru kwa upendo mkubwa, Rais John Magufuli ambaye aliendesha upatikanaji wa Visa katika Ubalozi wa Marekani siku ya Jumapili. Daktari Bingwa wa Mifupa wa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Elias Mashalla alisema anasikia raha kurejea nchini akiwa na watoto hao wakitembea licha ya kuondoka nao wakiwa katika machela.

Kwa upande wake, Dk Meyer kiongozi wa jopo la madaktari kutoka Marekani alisema Mungu ametenda muujiza wa uponyaji kwa watoto hao. Alisema licha ya kuwarudisha salama wameleta na vifaa mbalimbali vya kusaidia matibabu kwa wagonjwa.

Mjumbe wa Bunge la Marekani King alisema alipigiwa simu na Mkuu wa Samaritan’s Pass Bill Graham kumwomba msaada wa kuzungumza na serikali ya Marekani ili kuwasiliana na Ubalozi wa Tanzania kupata Visa kwenda Marekani kupatiwa matibabu watoto hao.

Katika mapokezi hayo walishiriki viongozi wa dini ambao ni Askofu Eliud Isangya wa Kanisa la Kimataifa la Evanglism na Shehve Mkuu wa Mkoa wa Arusha Shaban Juma na kuongoza sala ya kumshukuru Mungu kwa muujiza wa uponyaji.

Pia viongozi mbalimbali wa kisiasa, wanafunzi wa shule yao ya Lucky Vicent na wananchi walijumuika uwanjani hapo kuwapokea huku baadhi yao walitokea na machozi kwa furaha. Wakiwa eneo la Mbuguni kituo cha Steam walipokelewa na watoto wa shule za msingi mbalimbali waliotoa pongezi kwa ajili ya ujio wa watoto hao.