Manji mgonjwa, ashindwa kuhudhuria mahakamani

WAKILI wa Serikali, Esterzia Wilson ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mfanyabiashara Yusuf Manji ameshindwa kufi ka mahakamani hapo kwa kuwa anaumwa. Alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Alidai amepata taarifa kutoka Magereza kuwa Manji anaumwa na kwamba ana hati ya mapumziko ya siku mbili. Hata hivyo, alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 25, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa. Mbali na Manji, washitakiwa wengine ni Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda (28), Mtunza Stoo, Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43) mkazi wa Chanika ambao wote wanakabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi.

Inadaiwa Juni 30, mwaka huuu maeneo ya Chang’ombe A wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote kwa pamoja, walikutwa na askari polisi wakiwa na mabalo 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vyenye thamani ya Sh milioni 192.5.

Pia inadaiwa Julai Mosi mwaka huu, maeneo ya Chang’ombe A, wilayani Temeke, Dar es Salaam, washitakiwa wote walikutwa na askari polisi wakiwa na mabalo manane ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za JWTZ vyenye thamani ya Sh milioni 44.

Katika mashitaka ya tatu, inadaiwa Juni 30, mwaka huu maeneo ya Chang’ombe A, washitakiwa walikutwa wakiwa na mhuri wa JWTZ ambao uliandikwa ‘’Mkuu wa Kikosi 121 Kikosi cha JWTZ’’ bila kuwa na uhalali kitendo kinachohatarisha usalama wa nchi.

Pia inadaiwa, terehe hiyo hiyo maeneo ya Chang’ombe washitakiwa walikutwa na mhuri uliokuwa umeandikwa ‘’Kamanda Kikosi 834 KJ Makutupora Dodoma bila kuwa na uhalali kitendo kinachohatarisha usalama.

Ilidaiwa Juni 30, mwaka huu, maeneo hayo, washitakiwa kwa pamoja walikutwa na mhuri ulioandikwa ‘’Commanding Officer 835 KJ, Mgambo P.o.Box 224 Korogwe isivyo halali.

Katika mashitaka ya sita, inadaiwa Julai Mosi mwaka huu, maeneo hayo ya Chang’ombe, washitakiwa walikutwa na gari lenye namba za usajili SU 383 mali waliyojipatia isivyo halali