‘Kamatakamata’ ya vigogo yaanza

SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kuviagiza vyombo vya dola kuwashughulikia watuhumiwa waliotajwa kwenye kamati mbili za Bunge, zilizochunguza biashara za madini ya tanzanite na almasi nchini, baadhi ya watuhumiwa wamekamatwa na Polisi na wengine wanahojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Wakati Takukuru imesema ilianza kazi hiyo mara moja baada ya agizo la Rais juzi, Jeshi la Polisi limewakamata baadhi ya watuhumiwa waliotajwa kufanya vitendo vya kihalifu katika mikoa ya Arusha na Manyara na limewaagiza watuhumiwa wengine wote waliotajwa, kuripoti mara moja kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa mahojiano. Kamati hizo za Bunge ziliundwa na Spika Job Ndugai kwa ajili ya kuchunguza mazingira ya uchimbaji na biashara ya madini hayo; na kamati zote mbili zilibainisha kasoro nyingi, ikiwemo baadhi ya watendaji wa serikali kuhusika na uhujumu uchumi.

Akizungumza baada ya kupokea ripoti hizo, Rais Magufuli pamoja na kuagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi, aliwataka viongozi mbalimbali wanaotokana na uteuzi wake, waliotajwa kwenye kashfa hizo kukaa pembeni. Kutokana na agizo hilo, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, Naibu Waziri wa Ujenzi, Edwin Ngonyani na Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Elias Maswi walitangaza kujiuzulu.

Akizungumza na Habari- Leo jana, Msemaji wa Takukuru, Musa Misalaba alisema taasisi hiyo imeshaanza uchunguzi katika maeneo na hatua tofauti huku akisema inafanya kazi hiyo kwa kasi na umakini mkubwa. “Baada ya Rais kutoa agizo sisi kazi yetu ni kuchunguza na tumeshaanza kazi na tunaendelea nayo, uchunguzi unafanya kwa hatua na sisi tuko kwenye hatua mbalimbali, na tukimaliza tutatoa taarifa yetu rasmi,” alisema Misalaba.

Kwa upande wake, Jeshi la Polisi limewataka watajwa katika ripoti hiyo, kuripoti katika Ofisi ya DCI kwa ajili ya mahojiano huku likitangaza kuwakamata baadhi ya watuhumiwa. Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana alisema baada ya kupokea maelekezo ya Rais Magufuli, jana waliwakamata baadhi ya watuhumiwa katika mikoa ya Arusha na Manyara ambao wanahojiwa.

“Wale wote waliotajwa ofisi ya DCI imeshafungua jalada ni vizuri sana wao wenyewe wakajisalimisha ili waweze kuhojiwa na uchunguzi ufanyike tujue ni kwa kiasi gani wameshiriki katika suala hilo,” alisema Sirro. Alisisitiza kuwa lengo ni kuwatangazia wote waliotajwa kwenye sakata hilo la madini ya tanzanite na almasi, kwa busara na kujali heshima zao, wao wenyewe wakaripoti ili sheria ichukue mkondo wake.Alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine, tayari limeunda kikosi kazi cha kushughulikia ripoti hiyo kwa lengo la kukusanya ushahidi na hatimaye wahusika wafikishwe mahakamani.