Dereva wa Lissu, Mashinji wasakwa

WAKATI Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi, Kenya, Jeshi la Polisi limemtaka dereva wake, Adam na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji kuripoti Polisi Dodoma au Makao Makuu ya Upelekezi Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, SACP, Giless Muroto alisema jeshi hilo linamtaka devera wa Lissu na Katibu Mkuu wa Chadema kuripoti polisi ili kufanya mahojiano nao. “Popote alipo dereva wa Lissu, Adam ajitokeze na afike Polisi Dodoma na Makao Makuu ya Upelelezi Dar es Salaam ili kutoa maelezo kuhusiana na tukio kwani ndiye alikuwa pamoja na majeruhi,” alisema.

Kamanda alisema kitendo cha kutoweka kwa dereva huyo na kujificha ni kosa la jinai na kama kuna mtu au watu wanaomficha, wanatenda kosa la jinai, wamfikishe Polisi mara moja bila kukosa kwa kuwa ni shahidi muhimu katika upelelezi.

Kuhusu Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Mashinji, naye anatakiwa kuripoti kituo cha polisi kutokana na hotuba aliyotoa juzi, ambayo iliwahamasisha wanachama wa chama hicho popote walipo, kuwa wanatakiwa kuchangia damu, kitendo ambacho ni uchochezi, na kinaamsha mshituko katika jamii.

Akizungumzia upepelezi kuhusu Lissu kushambuliwa na risasi kati ya 28 hadi 32 na tano kumdhuru, Kamanda alitoa mwito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi.

Kamanda Muroto alisema Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na timu ya upelelezi kutoka Makao Makuu ya Upepelezi kutoka Dar es Salaam, linaendelea kufanya upelelezi wa kina ili kuwabaini waliohusika na tukio hilo.

“Pia taarifa zimetolewa mapema katika wilaya na mikoa jirani ili kufanya misako na ufuatiliaji kulingana na taarifa zilizopo ndani ya jeshi hilo,” alisema. Wakati upelelezi ukiendelea, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa sahihi ili kufanikisha kuwabaini watu waliohusika na tukio hilo la kumshambulia Lissu na matukio mengine.

Kamanda pia aliwaonya wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuandika habari za upotoshaji, uchochezi dhidi ya taasisi za serikali na baadhi ya viongozi wa dola kuhusu tukio hilo, kuacha mara moja.

Alitoa angalizo kwamba wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii, wanatenda kosa kisheria waanze kuchukua tahadhari wasije tumbukia mikononi mwa sheria. Aliwataka wale wote wenye taarifa sahihi kuhusu tukio hilo la kushambuliwa Lissu wajitokeze na watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi au kwa viongozi wa serikali walipo na taarifa hizo zitafanyiwa kazi ili kukomesha vitendo hivyo.

Aidha alisema jeshi hilo limeyakamata magari manane aina ya Nishani Patrol na yanafanyiwa uchunguzi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na taasisi nyingine kuhusiana na kuhusishwa na tukio la kujeruhiwa kwa risasi Mbunge Lissu.

Lissu ambaye ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alishambuliwa kwa risasi Septemba 7, mwaka huu saa 7.30 Area D katika maghorofa ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) katika Manispaa ya Dodoma.

Uchunguzi wa awali kuhusu tukio hilo, ambalo watu walioshambulia hawajulikani, Kamanda Muroto alisema unaonesha kuwa wahalifu walikuwa na silaha ya SMG/SAR kutokana na maganda ya risasi yaliyokutwa eneo la tukio.

Katika hatua nyingine, habari kutoka katika Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi ambako Lissu amelazwa zimeeleza kuwa, afya ya mbunge huyo imezidi kuimarika zaidi jana. Rais wa Chama cha Wanasheria nchini Kenya (LSK), Isaac Okero, alisema jana kuwa hali ya Lissu iliendelea kuwa imara zaidi jana kutokana na kufanyiwa upasuaji wa zaidi ya saa saba juzi.

Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), alishambuliwa akiwa ndani ya gari lake lenye namba T 216 DHH aina ya Toyota Land Cruiser rangi nyeusi lililokuwa likiendeshwa na dereva wake Adam.

Muruto pia alimpongeza Naibu Spika, Dk Ackson Tulia ambaye ni jirani yake Lissu, kwa kutoa msaada wa hali na mali pamoja na kutafuta PF 3 kwa ajili ya kupata huduma ya matibabu katika Hospitali ya Dodoma.

Katika kuhakikisha wananchi wanabaki watulivu, Kamanda Muroto pia alipiga marufuku mikusanyiko yoyote ya Chadema pamoja na mpango wa damu uliotangazwa na Dk Mashinji.

Polisi mkoani Dodoma pia imefanya msako mkali na kufanikiwa kukamata watuhumiwa 30 kwa makosa mbalimbali, yakiwemo kukutwa na misokoto ya bangi 862, na isiyosokotwa kilogramu 43, pombe haramu ya moshi lita 75 na mitambo ya gongo sita.

Kukamatwa wafuasi wa Chadema Ikungi Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraj Mtaturu amesema wafuasi 11 wa Chadema waliokamatwa juzi wilayani humo, walikamatwa kwa kosa la kukutwa na mabango ya uchochezi dhidi ya viongozi wa serikali.

Mtaturu alikanusha madai kuwa wafuasi hao, walikamatwa kutokana na kuendesha michango kwa ajili ya kuchangia matibabu ya Lissu, ambaye ni Mbunge wao. Alisema taarifa hizo za kupotosha, zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa wafuasi hao walikamatwa kwa kusa la kukusanya michango ya matibabu ya Lissu.

Aliomba umma kutupilia mbali upotoshaji huo wenye lengo la kuwafitinisha wana Ikungi na Jimbo la Singida Mashariki na kwamba waliokamatwa wote walihojiwa na baadaye kuachiwa kwa dhamana.

Alisema wilaya ya Ikungi inawalaani vikali wale wote waliohusika katika tukio hilo baya, linalokwenda kinyume na mila na desturi za Kitanzania na kumpa pole mbunge Lissu pamoja na wananchi wa Ikungi huku akimtakia uponaji wa haraka.

Kuhusu michango ya matibabu kutoka wilayani humo, alisema amemwagiza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ikungi kuitisha kikao cha madiwani wote na kuweka utaratibu wa pamoja wa jinsi ya kuchangia matibabu ya mbunge wao.

Bavicha kuisaidia Polisi Wakati huohuo Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA) limesema liko tayari kutoa taarifa muda wowote kwa Jeshi la Polisi nchini, kuhusu wahalifu mbalimbali wanaohusika katika matukio ambao wanashindwa kubainika na kuchukuliwa hatua.

Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia mikakati mbalimbali iliyopangwa na Baraza hilo kwa ajili ya kupambana na wahalifu wanaodaiwa kutojulikana wanaohusika katika matukio.

“Watu wasiojulikana wameendelea kulisumbua Jeshi la Polisi hata vyombo vya sheria kuwa kutojulikana na kuchukuliwa hatua, haiwezekani ifikie wakati wajulikane na hatua zichukuliwe,” alisema na kuongeza kuwa kitendo cha kupigwa risasi kwa Lissu kinaweza taifa katika wakati mgumu.

Alisema Baraza hilo liko bega kwa bega na vyombo vya ulinzi na usalama muda wowote wa saa 24 kwa mwaka ili kutoa taarifa na kusaidia ili wahalifu hao waweze kupatikana na hatua nyingine za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

Alisema Baraza hilo linakubali kuanza kutoa taarifa hasa ikizingatiwa kuwepo kwa baadhi ya matukio ambayo yamekuwa yakitokea huku Jeshi la Polisi likidai kutowafahamu waliohusika na matukio hayo ambayo ni ya kihalifu.

Katibu wa Bavicha, Julius Mvita alisema ni wajibu wa serikali kuchukua hatua za haraka, vyombo vya ulinzi na usalama kujitokeza na kusema jambo ikizingatiwa kuwa walipewa taarifa kuhusu mashaka ya usalama wa maisha.