Vigogo wastaafu polisi wampa mbinu Sirro

VIGOGO wastaafu wa Jeshi a Polisi wamekutana na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kumpa mbinu mbalimbali za kudhibiti uhalifu nchini ikiwa ni pamoja kumtaka akae chonjo na wanasiasa.

Kikao hicho kilifanyika jana jijini Dar es Salaam, ambapo Sirro alikutana na Wakuu wa Jeshi hilo wastaafu, makamishna na manaibu waliostaafu, walioko kazini na wale waliopangiwa kazi katika idara nyingine lengo ikiwa ni kujadili mambo mbalimbali kuboresha kazi za jeshi hilo.

Sirro alisema lengo ni kufahamiana na kukumbushana kazi pamoja na kupata ushauri kutoka kwa wazoefu hao. “Wazee wetu waliostaafu hawa walikuwa wanatukumbusha mambo ya msingi na hasa weledi, kwamba wakiwa huko wanatuangalia wanaona kuna mapungufu kwa baadhi ya askari wetu na pia wametusisitiza mafunzo,” alisema Sirro.

Alisema ili jeshi liwe imara ni muhimu kutoa mafunzo mbalimbali na hasa yale ya kazi maalumu kama vile kesi za kimtandao ili jeshi liendane na wakati. Alisema pia imesisitizwa jeshi hilo kuendelea kuwa karibu na wastaafu katika jeshi hilo kupata ushauri wa kikazi ambapo wastaafu wameahidi kuendelea kutoa ushirikiano na hasa katika kutoa ushauri wa maboresho ya kazi.

“Wazee wetu hawa wamefanya kazi kwa muda mrefu, kwa hiyo ukimwita anakuwa na ujuzi wa kutosha ambao utatusaidia sana, na tumekubaliana kila baada ya miezi miwili au mitatu tutakuwa tunakutana ili tuendelee kujirekebisha,” alisema Sirro.

Naye Mkuu wa Jeshi hilo mstaafu, Omari Mahita alisema changamoto kubwa ya kwanza kwa jeshi hilo kwa sasa ni wanasiasa na kwamba mikakati waliyoiweka anaamini yatasaidia kuboresha kazi ya jeshi la polisi.

“Niwe muwazi tu changamoto ya kwanza ni namna ya kushughulika na wanasiasa, ni kazi kubwa sana ku deal nao, kwa mikakati tuliyoiweka tutaenda tu,” alisema. Mahita katika uongozi wake katika jeshi hilo alikuwa maarufu kwa jina la ‘ngunguri’ kutokana na kauli yake alipokuwa akikabiliana na wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), alikuwa akisema kama viongozi wa chama hicho wako ‘ngangari’, basi jeshi la polisi liko ‘ngunguri’ kukabiliana nao.

Hivi karibuni pia Mahita alinukuliwa na vyombo vya habari kuwa uhalifu katika vituo vya polisi ni dhahiri kuwa polisi imekosa kuungwa mkono, hivyo kupunguza ufanisi wake katika kutekeleza majukumu yake.

Aidha Mahita alikaririwa pia akikosoa kitendo cha askari polisi kuwa wapole na kueleza kuwa mhalifu habembelezwi. Aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu alisema wastaafu ni watu sahihi wa kutoa ushauri kwa jeshi hilo kuboresha kazi zao.

“Sisi tuliokuwa watumishi wa jeshi hili ni kioo, tunayosikia na kukutana nayo ni vizuri tuwafikishie ili waboreshe utendaji wao ili waweze kuboresha utendaji wao wakidhi matarajio ya jamii Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu, Inspekta Jenerali Saidi Mwema alisema kikao hicho, ambacho muasisi wake ni Rais John Magufuli kitasaidia kuweka mikakati mbalimbali ndani ya jeshi hilo ili kuzuia uhalifu nchini, ambapo amempongeza sana IGP Sirro kwa kuamua kukutana nao.