Wafungwa China kuanika mtandao dawa za kulevya

KUTOKANA na uhusiano mzuri kati ya Tanzania na China, Tanzania imeruhusiwa kutuma ujumbe wake katika nchi hiyo kutembelea wafungwa wa kesi za dawa za kulevya waliofungwa China na kufanya nao mahojiano ili kuupata mtandao mzima wa biashara hiyo.

Kamishna wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Siyanga alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilipoandaa shughuli ya kumuaga Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing ambaye amemaliza muda wake.

“Tumepanga kutembelea jela nchini China kuzungumza na Watanzania ambao wamekamatwa huko kwa makosa ya dawa za kulevya ili tuweze kunasa mtandao mzima,” alieleza Siyanga na kuongeza kuwa anaamini kwamba vijana waliokamatwa na kufungwa China, pengine kuna waliostahili adhabu hiyo na pengine zaidi kwani ndio wahusika wakuu katika biashara hiyo hatari, lakini bado wako uraiani.

Aliishukuru pia China kwa misaada wake kwa Tanzania katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, kwani imetoa nafasi ya mafunzo kwa watumishi wa taasisi hiyo kwenda kujifunza nchini kwao ambao watano wamekwishaondoka na wiki hii 15 watakwenda.

Pia wametoa vifaa kama kompyuta na magari. “Nyie ni mshumaa kwetu, tunapenda muendelee kuangaza, usaidie katika hilo kwa sababu tunapambana na dawa za kulevya hatutaki vijana wetu wasio na hatia waharibike kwa dawa za kulevya,” alisema Kamishna Siyanga na kuongeza kuwa Tanzania itaendelea kukumbuka misaada mbalimbali ambayo ilipatikana kutoka China katika uongozi wa balozi huyo akiwa nchini na hasa katika kutokomeza dawa za kulevya.

Balozi Lu alishauri nchi hizo mbili ziendelee kujenga uhusiano katika kupambana na dawa za kulevya na kuahidi kupeleka pendekezo la kuingia makubaliano rasmi kwa waziri anayeshughulikia masuala hayo nchini China. Alisema China na Tanzania zina uhusiano mzuri na kwa karibu ambapo moja na mshikamano ni katika kupambana na dawa za kulevya.

Alimpongeza Rais John Magufuli kwa kusimama kidete kupambana na usafirishaji wa dawa za kulevya ambazo zinaharibu afya za watu, sifa ya nchi pamoja na nguvu kazi. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga alisema balozi huyo alikuwa kiungo kizuri kati ya China na Tanzania na kwamba katika kipindi chake mambo mengi mazuri yalifanyika, ikiwa ni pamoja na kusaidia mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

“China imetusaidia mafunzo na vifaa, lakini pia Watanzania wengi wako katika jela huko China, wakikamatwa kutoka nchi nyingine wananyongwa, lakini kwa Tanzania wengi wao hawajafanyiwa hivyo wamefungwa vifungo virefu au maisha, bado tunazungumza ni adhabu gani wanaweza kupewa hapa nchini au huko,” alieleza Dk Mahiga.