Kuharibu miundombinu ya reli faini milioni 70/-

WAKATI Serikali imeshaanza kujenga reli mpya ya viwango vya kimataifa yenye urefu wa kilometa 2,561, imewasilisha Muswada wa Sheria ya Reli bungeni wenye lengo la kusimamia, kulinda na kuendeleza miundombinu ya reli, ambao unaweka adhabu inayofi kia Sh milioni 70 kwa waharibifu wa miundombinu hiyo.

Kitu kikubwa katika muswada huo ni ukali wa adhabu kwa wananchi na wafanyakazi kuhusu matunzo na uendelezaji wa reli pamoja na treni. Baadhi ya makosa yaliyoainishwa ambayo adhabu yake ni mpaka Sh milioni 70 ni matumizi ya ardhi ya dharura bila ridhaa ya shirika, kuhatarisha usalama wa maisha ya watu wanaosafiri na treni au walio katika reli, kuweka au kutupa vitu hatarishi katika miundombinu ya reli kama vile mbao na mawe, ulevi kazini, kughushi tiketi, kusafiri bila tiketi, kusafirisha bidhaa hatarishi kinyume cha utaratibu na wafanyakazi wanaohatarisha usalama wa huduma za reli.

Muswada huo unaotarajiwa kujadiliwa bungeni keshokutwa Jumatano baada ya kipindi cha maswali na majibu, unaletwa bungeni miezi mitano baada ya Rais John Magufuli kuzindua ujenzi wa reli viwango vya kimataifa. Aliifanya kazi hiyo Aprili mwaka huu.

Aidha, muswada huo ambao ukipitishwa utaondoa miswada mingine, huku ikibakiza vipengele muhimu, unafafanua pamoja na mambo mengine utoaji wa huduma za usafiri na adhabu mbalimbali kwa wale ambao wataonekana kuhujumu Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) wakiwamo wananchi na wafanyakazi.

Katika eneo la adhabu, faini zake ni kuanzia Sh milioni tano kwa makosa hatarishi ya njia ya reli na treni hadi Sh milioni 70, huku adhabu zinazogusa utendaji wa kazi zinacheza kati ya Sh milioni mbili hadi Sh milioni tano pamoja na vifungo jela.

Muswada huo unatoa mamlaka kwa shirika kutwaa ardhi kwa ajili ya matumizi ya miradi ya reli, kulinda pia njia za reli na maeneo ya dharura na matumizi ya akiba ya ardhi. Kama muswada huo utapita na kuwa sheria, utaleta mabadiliko mengi, ikiwamo kufuta Sheria ya Reli ya Mwaka 2002 ambayo ilitumika pia kuanzisha Shirika Hodhi la Mali za Reli (RAHCO) na TRL mwaka 2012 ambayo pia ilielekeza mdhibiti kuwa ni Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).

Kutokana na kufutwa kwa shirika hodhi na TRL, kutakuwapo na kujipanga upya kwa wafanyakazi ambapo watumishi wa Rahco na TRL wanaokidhi vigezo watahamishiwa katika shirika jipya na wengine katika wizara au taasisi mbalimbali za umma.

Aidha, katika sheria hiyo kumeelezwa kuwa watumishi ambao hawatahamishiwa katika shirika jipya, wizarani au taasisi nyingine za umma, ajira zao zitasistishwa na watalipwa stahiki zao zote kwa mujibu wa sheria na kwa kuzingatia masharti na vigezo vya ajira zao.

Mambo mengine kwenye sheria hiyo ni mamlaka yaliyotolewa kwa Waziri anayehusika kuunda kampuni nyingine ndogo ya kutoa huduma kama ikibidi. Katika maeneo ya adhabu wakati sheria nyingi zilizopita zilikuwa zinaanzia Sh milioni moja na kusimama katika Sh milioni nne, sheria mpya inaanzia Sh milioni mbili huku kiwango cha juu ni Sh milioni 70; wakati adhabu nyingine kama kukalia eneo la reli na akiba yake faini ikiwa inacheza kati ya Sh milioni 10 hadi Sh milioni 20.

Muswada huo unatoa adhabu ya mtu yeyote yule anayezuia treni kutumia reli ama kwa uzembe, kinyume cha sheria faini ya Sh milioni 50, lakini isizidi Sh milioni 70 na adhabu ya kwenda jela juu ya miaka mitatu, lakini isizidi mitano au vyote viwili.

Matendo yanayoelezwa kuwa ni kuzuia treni isitumie reli ni pamoja na kuweka vitu mbalimbali katika njia ya reli kama miti mawe; kwa kunyofoa vifaa vya reli; kuharibu njia ya reli au kuitia moto au kufanya kitu chochote kile ambacho kitaharibu au kuzuia treni isitumie njia ya reli au treni yenyewe kuharibika.

Pia kwa mtu ambaye atapatikana na kifaa cha treni au reli kinyume cha sheria atakabiliwa na faini ya Sh milioni tano na si zaidi ya Sh milioni 10 na kifungo cha miaka mitatu na kisichozidi mitano au adhabu zote mbili. Pia kuna adhabu kwa mtu anayesaidia au kumsaidia mtu mwingine kufanya uharibifu.

Pia mfanyakazi atakayeingia kazini akiwa amelewa akapimwa na kubainika kiwango chake cha ulevi, atatozwa faini isiyozidi Sh milioni tano, ya chini Sh milioni mbili au kwenda jela miezi 18 au vyote viwili. Pia watakaosafirisha vitu vya hatari bila kibali watalambwa faini ya isiyozidi Sh milioni 10, ya chini milioni tano au kifungo miaka miwili.

Kwa wale watakaobambwa wanasafiri bila tiketi halali ya TRL watalazimika kulipa faini ya Sh zisizozidi 500,000 au jela miezi mitatu wakati mwenye tiketi ya kufoji atatozwa faini ya Sh milioni tano au si zaidi ya Sh milioni 10 ama jela miaka miwili au zaidi, lakini isiyozidi mitano.

Kwa wafanyakazi, watakabiliwa na adhabu ya faini ya Sh milioni tano au isiyozidi milioni 10 au kutupwa jela miaka isiyozidi mitano kwa ama kuomba rushwa au kutaka fedha zaidi ya sheria au anayevuruga usalama. Ukiangalia adhabu kali zilizowekwa zimelenga kuhakikisha miundombinu na huduma inakuwa salama katika kiwango kinachotakiwa