Jaji Mkuu Mteule: Walete kortini ‘watu wasiojulikana’

JAJI Mkuu Mteule, Profesa Ibrahim Juma amezitaka mamlaka za upelelezi nchini kufanya kazi zao na kutoa majibu ya uhakika, kwa kuwa haipendezi kuona watu wanaofanya makosa kisha kutokomea wakipewa jina la watu wasiojulikana.

Profesa Juma alisema msamiati huo wa watu wasiojulikana, unawafanya wananchi kuanza kutoa tafsiri tofauti alizoziita za kisiasa na hivyo kuvitaka vyombo vya upelelezi kuwafikisha watuhumiwa mahakamani ili kujenga imani kwa jamii.

Profesa Juma (59) aliyasema hayo alipozungumza na gazeti hili jana mchana baada ya Rais John Magufuli kumteua kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania. Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu jana, Rais Magufuli amemteua Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania kuanzia jana.

Alikuwa akikaimu nafasi hiyo kuanzia Januari 18, mwaka huu, akiwa amechukua nafasi ya Mohamed Chande Othman ambaye amestaafu. Ataapishwa leo saa 4:00 asubuhi, Ikulu jijini Dar es Salaam. “Waliopewa dhamana ya upelelezi wafanye kazi zao, lakini pia tutumie mifumo ya kisasa ya kiusalama kama vile kufunga kamera barabarani kama ilivyo kwenye miji mingine ya Nairobi na London ili iwe rahisi kujua namba za magari yanayotumika kufanya uhalifu lakini pia kupata sura za wahalifu hao,” alieleza Jaji Mkuu.

Kuhusu usalama wa mawakili, Jaji Mkuu Mteule alisema mawakili wanapokuwa nje ya mahakama wana haki ya kuwa salama kama raia mwingine yeyote, hivyo haileti picha nzuri kwa wanasheria kushambuliwa.

Alisema wananchi wanapenda kuona Polisi wakifanya kazi zao kisayansi na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani. Aidha, Profesa Juma alisema kuna tatizo kubwa kwa Watanzania kujitokeza kutoa ushahidi polisi au mahakamani pale wanapotakiwa kufanya hivyo.

Alisema utakuta watu wakieleza vizuri kwenye televisheni inapotokea ajali, lakini wanapotakiwa kutoa ushahidi wanakimbia. Kwa mujibu wake, kutoa ushahidi ni wajibu wa kiraia, hivyo jamii inapaswa kuelewa kuwa mashahidi siyo watu wabaya na wananchi wanapaswa kuiamini mahakama.

Alisema wananchi pia wanaweza kutoa ushahidi wa picha za matukio ya uhalifu wanazopiga au sauti wanazorekodi kupitia simu zao za mkononi kwani nao unakubalika mahakamani. Kuhusu changamoto za mahakama, Jaji Mkuu Mteule alisema mahakama ina Mpango Mkakati wake wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2015-2020) ambao atausimamia ili ufanikiwe.

Alisema anafahamu kuwa kuna upungufu wa majaji, mahakimu, makarani na majengo ya mahakama nchini mambo ambayo atayafanyia kazi. Alisema ataiomba Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), itoe kibali cha ajira ili mahakama iajiri watumishi wapya, lakini pia ataiomba mamlaka ya uteuzi iongeze idadi ya majaji.

Alisema kuna mpango pia wa kujenga Mahakama Kuu Kigoma na Morogoro na mahakama za Wilaya na Mwanzo maeneo mbalimbali ya nchi na kusema mpaka ifikapo mwaka 2020, mahakama itakuwa na sura mpya.

Profesa Juma anaamini kwenye dhana ya umoja ni nguvu na hivyo amewaomba watendaji wote kwenye mhimili wa Mahakama na wananchi kumpa ushirikiano na wawe kitu kimoja kwa kuwa dhamana aliyopewa na Rais ya kuongoza mhimili huu ni kubwa hivyo anahitaji ushirikiano wa kila mmoja.

Profesa Ibrahim Hamisi Juma alizaliwa Juni 15, 1958, Musoma mkoani Mara. Kabla ya kuteuliwa kuwa Kaimu Jaji Mkuu, alikuwa jaji katika Mahakama ya Rufaa Tanzania. Aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na Rais Jakaya Kikwete, mwaka 2008, kabla ya kupandishwa na kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa mwaka 2012.

Pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT). Alisoma sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Shahada ya Kwanza na ya Pili), Shahada ya Uzamili Chuo Kikuu cha Raoul Wallenberg, Lund nchini Sweden akijikita katika Sheria za Kimataifa za Haki za Binadamu, na Shahada ya Udaktari wa Falsafa (Phd) ya Chuo Kikuu cha Ghent nchini Ubelgiji, akijikita katika Sheria za Bahari.

Anasifika kwa kuwa mbobezi katika masuala hayo ya sheria za bahari, haki za binadamu, sheria za wakimbizi na sheria za mazingira. Anakuwa Jaji Mkuu wa nane wa Tanzania akitanguliwa na 1964–1965: Ralph Windham (1964-1965), Philip Georges (1965-1971, Augustine Saidi (1971-1977), Francis Nyalali (1977– 2000), Barnabas Samatta (2000–2007), Augustino Ramadhani (2007–2010), na Mohamed Chande Othman (2010–2017).