‘Viachieni vyombo vya ulinzi kuchunguza upigwaji Lissu’

WATANZANIA wametakiwa kuvipa nafasi na muda vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza kwa undani na umakini suala la kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.

Lissu, ambaye ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alishambuliwa kwa risasi Septemba 7, mwaka huu saa 7.30 Area D katika maghorofa ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) katika Manispaa ya Dodoma.

Rai hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matamko yanayotolewa na watu mbalimbali kuhusu tukio la kupigwa risasi na watu wasiofahamika kwa mbunge huyo.

Shaka alisema tangu kutokea kwa tukio hilo, watu mbalimbali ikiwemo Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA), wamekuwa wakitoa matamshi mbalimbali ya kebehi yanayojenga utata na mkanganyiko.

“Sehemu kubwa katika maelezo ya viongozi hao kwa nyakati tofauti hayakuonesha ukomavu, busara wala hekima ukilinganisha na ukubwa wa tatizo la kushambuliwa kwa Lissu, huku wakidhani jambo hilo limewafurahisha watanzania ila linawauma Bavicha kuliko wananchi wengine,” alieleza.

Aliongeza kuwa tukio la kushambuliwa Lissu na watu wasiojulikana ni jambo dogo kama wanavyochukulia hivyo ni vyema wakaviacha vyombo vya ulinzi vikafanya kazi yao na kisha kulitolea suala hilo maelezo.