Muswada watua bungeni Dodoma kuifuta Rubada

SERIKALI imewasilisha bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 3 wa Mwaka 2017, ambao pamoja na mambo mengine, unapendekeza kufutwa kwa Mamlaka ya Uendelezaji ya Bonde la Mto Rufi ji (Rubada) iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge 1975, kutokana na majukumu yake ya kisheria kutekelezwa na taasisi nyingine.

Hoja ya kutaka kufutwa kwa mamlaka hiyo ambayo ilianzishwa kwa nia ya kusimamia, kuratibu kuwezesha maendeleo yenye maendeleo endelevu yenye kuangalia ikolojia kupitia bonde hilo katika sekta ya nishati, kilimo, uvuvi misitu, utalii, madini, viwanda, usafirishaji na mazingira, imo katika muswada huo.

Muswada huo ulisomwa kwa mara ya kwanza Jumanne iliyopita na kesho utaletwa tena bungeni. Kama mapendekezo hayo ya serikali yatapita, maana yake wafanyakazi wa Rubada watapelekwa katika mamlaka nyingine za umma.

Aidha, kwa mujibu wa sheria hiyo mpya kama itapita, wale ambao hataingizwa katika wizara mbalimbali kufanya kazi ya utumishi wa umma watalipwa stahiki zao zote kabla ya kuachishwa kazi.

Aidha, ndani ya muswada huo, shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na taasisi hiyo sasa zitapelekwa katika wizara inayohusika na Mipango na Maendeleo. Pia muswada huo unaonesha kwamba baada ya wizara husika kukabidhiwa, itamuita wenzake wa kilimo ili kuangalia namna ya kukagawana mali na madeni husika.

Ikijinafasi katika kuwa taasisi yenye ushindani kuendeleza uchumi wa Bonde la Rufiji kwa kuzingatia mazingira; kazi yake kubwa ikiwa ni kuuza, kudhibiti, kuratibu na kuwezesha maendeleo ya muda mrefu katika jamii, inafutwa kutokana na kuwapo na mabadiliko ya kisera ambayo yameifanya Rubada kukosa umuhimu wa kuendelea kuwapo, kupigwa kwake mwereka kunatokana na kushindwa kukidhi vigezo vya kuendelea kuwa hai.

Shughuli nyingi ambazo zipo katika mpango mkakati wa taasisi hiyo uliotengenezwa mwaka 2013 na unaotarajiwa kukamilika mwaka huu, zinaonekana kuchukuliwa na taasisi nyingi na yenyewe kukosa nguvu.

Shughuli hizo ni uzalishaji umeme na kilimo cha kisasa katika Bonde la Mto Rufiji huku suala la mazingira likiangaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lililo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.

Mpango mkakati huo uliokuwa unaanza 2013 hadi 2017 na kupitishwa na Bodi ya taasisi hiyo Aprili 27, 2013, pamoja na mambo mengine ni kushawishi ubia ambao utawezesha kufanya miradi yake mikubwa ya umeme na kilimo huku ikisaidia Ukanda wa Maendeleo ya Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) katika kazi zake.

Ikiwa inaamini kwamba yenyewe ndiyo itakayobaki kuishauri serikali na kuendelea kuratibu na hivyo kupata fedha zaidi za serikali ili kutekeleza mpango wa kupunguza umaskini wa kitaifa (NSGRP), Sagcot na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambayo tayari imeshafutwa mpango mkakati huo ulitarajia fedha za serikali wanazopewa Rubada kuongezeka kufikia Sh 6,524424,806.40 kwa mwaka huu kutoka Sh 3,508,248,350 zilizopitishwa na Bodi ya Wakurugenzi mwaka 2013.

Mwaka 2015, akizungumza na gazeti moja la Kiingereza nchini, Mkurugenzi wa Rubada wakati huo alisema kunaandaliwa mabadiliko ya sheria ili kuwezesha Rubada kuingia katika mradi wa kufua umeme, Stiegler’s Gorge ambako bwawa lake lilitakiwa kujengwa kukidhi shughuli anuai.

Kuna taasisi nyingi zilizoanzishwa kwa mujibu wa sheria ambazo zimekuwa zikifanya kazi ambazo awali ilionekana kutakiwa kufanywa na Rubada ambayo kufikia mwaka 1984 walikuwa wameshakamilisha ramani ya maeneo ya kufua umeme katika Bonde la Mto Rufiji wakisaidia na Kampuni ya Canada ya NorConsult.

Katika uhai wake, Rubada katika kilimo ilishawahi kufanya upembeuzi Rufiji ya Chini na kuangalia maeneo oevu na kubaini kwamba kunawezwa kulimwa mpunga. Rubada pia ina miradi miwili ya umwagiliaji Rufiji na Kilombero. Miradi hiyo inafanyiwa kwa ushirikiano na mataifa ya Korea na Iran.

Muswada unaowasilishwa kesho ndani yake kutakuwa na urekebishaji wa sheria 12 zikijumuishwa Sheria ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam, Sheria ya Elimu, Sheria ya Mtoto, Sheria ya Madini, Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji, Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusu Rasilimali za Nchi na Sheria ya Petroli.

Nyingine ni Sheria ya Sumatra, Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Sheria ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Sheria ya Mipango Miji na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani