Katibu Mkuu Chadema ahojiwa, kisa Lissu

KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji ameripoti katika Ofi si ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na kueleza kuwa hawafahamu watu waliompiga risasi Mwanasheria wa chama hicho na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Dk Mashinji aliyehojiwa na maofisa wa polisi jana kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 9 alasiri, alisema maofisa wa Polisi walitaka kujua kama anafahamu watu waliomshambulia Lissu. Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili, kiongozi huyo alieleza kuwa Polisi walihisi anawafahamu waliohusika na tukio hilo baada ya kuzungumza na waandishi wa habari.

“Niliwaambia maofisa wa Polisi warejee katika mazungumzo yangu na waandishi wa habari ili kuona kama kuna dalili ya kuwafahamu, lakini mimi siwafahamu, bali niliwataka wananchi kuwafufua polisi jamii ambao watasaidia kuimarisha ulinzi,” alisema Dk Mashinji.

Alidai baada ya kuwaambia hivyo, waliangalia mazungumzo yake na kubaini kuwa katika kauli zake hajaonesha kama alikuwa anawajua watu hao. Pia alisisitiza kuwa maofisa hao wa polisi walitaka kujua kama anazo taarifa zozote kuhusiana na tukio na kueleza kuwa hana taarifa hizo.

“Nawaomba Polisi kuhakikisha waliofanya tukio hilo wanakamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria,” alisisitiza. Saa tano asubuhi kiongozi huyo alifika katika ofisi hizo huku waandishi wa habari wakizuiliwa kuingia ndani na hata kukaa nje ya ofisi hiyo.

Hata hivyo, gazeti hili lilipomtafuta kwa njia ya simu DCI Robert Boaz alisema yupo kwenye kikao hivyo baada ya dakika 20 atafutwe, lakini baadaye alisema yupo safarini kuelekea Dodoma.

Pia, simu ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro haikupokelewa alipotafutwa kuelezea suala hilo. Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa Dodoma na kupelekwa chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na sasa anapatiwa matibabu Nairobi nchini Kenya.

Wakati huo huo, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja ametii mwito wa IGP uliowataka kuripoti kwa DCI kutokana na kutajwa kwenye sakata la madini ya almasi na tanzanite. Waziri huyo wa zamani wa Nishati na Madini alihojiwa kwa saa moja na baada ya kutoka, alikataa kuzungumza na wanahabari kuhusu mahojiano waliyofanya.