Rais Magufuli amfariji Meja Jen. Mribata Lugalo

RAIS Dk John Pombe Magufuli amemtembelea Meja Jen. Mstaafu Vincent Mribata aliyelazwa katika hospitali ya Lugalo baada ya kushambuliwa na watu wenye silaha wakati akiingia nyumbani kwake Ununio katika Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam.

Meja Jenerali Mribata alishambuliwa kwa risasi jana tarehe 11 Septemba, 2017 na kukimbizwa katika hospitali ya Jeshi Lugalo kwa matibabu. Mkuu wa Kituo cha tiba cha hospitali hiyo na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo Brigedia Jenerali Paul Massawe amemueleza Rais kuwa mgonjwa anaendelea vizuri baada ya madaktari kufanikiwa kutoa risasi zilizokuwa mwilini katika sehemu za mkononi, kiunoni na tumboni.

Rais Magufuli ambaye aliambatana na Mkuu wa Majeshi nchini Jenerali Venance Mabeyo ametembelea pia wodi ya majeruhi na kuwajulia hali wagonjwa waliokuwa katika wodi hiyo.

Rais Magufuli amewapongeza madaktari wa hospitali ya jeshi ya Lugalo kwa huduma za matibabu wanazotoa kwa askari na wananchi kwa ujumla. Rais Magufuli amewahakikishia kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono kwa kufanyia kazi changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.