Bunge labariki bomba la mafuta Hoima-Tanga

BUNGE limepitisha azimio la kuridhia mkataba wa Serikali ya Tanzania na Uganda kuhusu mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima Uganda hadi Chongolieni, Tanga kwa kuweka angalizo kuhusu kodi na fi dia kwa wananchi.

Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Azimio la Bunge la kuridhia mkataba huo wa kimataifa, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deogratius Ngalawa alisema serikali inatakiwa kuwa makini na kifungu cha 2(c) cha Sehemu B ambayo inahusu kodi ya makampuni.

Ngalawa ambaye ni Mbunge wa Ludewa (CCM), alisema kifungu hicho kinaweza kutumiwa na wawekezaji wasiokuwa waaminifu kuihujumu nchi. Kwa mujibu wa Ngalawa, kifungu hicho kinaruhusu hasara iliyobainika katika utekelezaji wa mradi kabla, wakati au baada ya kipindi cha msamaha wa kodi kusogezwa mbele katika mwaka wa fedha unaofuata iwapo haikufanyiwa kazi katika mwaka wa fedha husika.

“Kamati inashauri serikali iwe makini na kifungu hiki wakati wa utekelezaji wa mradi ili kampuni zitakazohusika kutekeleza mradi zisijaribu kukitumia kutangaza kupata hasara kila mwaka, na hivyo kuikosesha serikali mapato stahiki,” alieleza.

Aidha, kamati hiyo pamoja na kumpongeza Rais John Magufuli kwa kuwezesha bomba hilo kupita nchini na hivyo kutoa fursa nyingi za ajira na kipato kwa serikali na wananchi, waliishauri serikali kuangalia kwa umakini Ibara ya Saba ya Mkataba ambayo inaruhusu kampuni itakayoitekeleza mradi kusafirisha fedha nje ya Uganda na Tanzania na kuzihifadhi huko bila kizuizi chochote.

“Kamati inaishauri serikali kuangalia kwa umakini ibara hii ili kuepuka kukinzana na sheria ya mamlaka ya nchi kuhusiana na umiliki wa mali asili ya mwaka 2017, alieleza. Sheria hiyo inazuia wawekezaji wa kusafirisha fedha kwenda nje ya nchi isipokuwa zile zinazotokana na mgawo wa faida inayopatikana.

Nayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bunge ilitaka kuwepo na upembuzi yakinifu wa mradi kabla ya kuingia katika makubaliano ya utekelezaji. Walitoa kauli hiyo huku wakisifu juhudi za Rais kuuleta mradi huo Tanzania.

Katika hotuba iliyosomwa na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-Wizara ya Nishati na Madini, Devotha Minja, Wapinzani walisema lingekuwa jambo la busara kwa bunge kutoridhia azimio hilo hadi pale mkataba utakapopitiwa vizuri na kujiridhisha na vifungu.

Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa na wabunge wengine waliochangia ambao walitoa angalizo na usahihi kwamba mkataba unaozungumzwa si mkataba, bali ni azimio ambalo inatakiwa kuzingatia masharti ya kimataifa.

Pamoja na hotuba yao kutolewa ufafanuzi na Waziri Harrison Mwakyembe kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria waliowasilisha Azimio hilo, wapinzani walikuwa na hoja mbalimbali za ushirikishaji wananchi, fidia na kuonya kwamba bunge lisiingizwe kwenye mtego wa kutunga sheria zinazokinzana.

Dk Mwakyembe hata hivyo alisema hakuna sheria zinazokinzana katika mkataba huo kwa kuwa Watanzania ni wasafirishaji wa mafuta ya Uganda, wakitumika kama vile lori linalobeba ndizi kutoka Kyela kwani ndizi hizo si za mwenye lori.

Wapinzani pia walizungumzia kadhia ya utoaji ardhi na kusema lazima ufanyike katika mazingira yenye manufaa kwa wananchi na kwamba ardhi iuzwe katika thamani ya soko. Mbunge Musa Mbarouk wa Tanga Mjini (CUF) pamoja na kuunga mkono hoja za wapinzani, alitoa ushauri kwa serikali kufanya maandalizi ya kuishirikisha wananchi na kuwa makini katika kila hatua kwa ajili ya usalama wa mradi wenyewe.

Aidha, alitaka malipo ya fidia yanapaswa kuangaliwa upya kwa kuwa wengi wa wananchi akitolea mfano wa jimboni kwake ambako bandari ya Chongoleani inajengwa wanapoteza ardhi ambayo ni tegemeo lao kubwa. Alisema wananchi hao wanastahili kupelekwa katika maeneo mengine kama shamba la katani la Amboni ambalo halijaendelezwa.

Alisema wananchi wa Chongoleani wanategemea kilimo cha minazi na matunda kuishi na kuondolewa kwao eneo hilo na fidia ndogo haitawasaidia. Alishauri pia wawakilishi wa wananchi katika maeneo ambalo bomba hilo litapita washiriki kikamilifu ili kuwatetea wananchi wao wasije wakarejea katika dimbwi la umaskini.

Bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,445 Tanzania likiwa na kilomita 1,149 litapita katika mikoa nane, wilaya 24 za Tanzania Bara. Naye Profesa Anna Tibaijuka wa Muleba Kusini (CCM), aliridhia azimio hilo huku akiwataka watu wasichanganye kati ya mikataba ya serikali na kampuni na serikali kwa serikali.

Aidha, amemtaka waziri mwenye dhamana ya ardhi kuondoa utata unaofanywa sasa na wapima ardhi wanaopima maeneo yakatakayopita bomba bila taarifa hata kwa mbunge anayehusika. Aliuliza kama hao wanafanya leo, na hao wa mafuta watakapofika si itakuwa mtafuruku mkubwa, alihoji mbunge huyo.

Amewataka wananchi kuimarisha ulinzi wa bomba hilo litakapojengwa na pia kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na uwepo wake. Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), alitaka wananchi walipwe fidia stahiki kwa wakati muafaka na kutaka pia madiwani na wabunge kushirikishwa katika maeneo yatakayopita bomba na kutaka sasa miundombinu itakayosaidia ulinzi wa bomba hilo kama barabara inayotokea Tanga na kupita mkoani kwake kufanyiwa kazi.

Bomba hilo kutoka Hoima, Uganda linapita katika wilaya ya Chemba kwa kilometa 170. Mbunge wa Musoma Mjini, Vedastus Manyinyi (CCM) alisema mipango ifanyike ili bomba hilo liwe moja ya miundombinu inayochangamsha fursa za kiuchumi.

Akifunga mjadala Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Mwakyembe kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Pro- INATOKA UK.3 fesa Palamagamba Kabudi, alisema pamoja na faida zilizopo wazi katika mradi huo, Watanzania wenyewe wanatakiwa kuchangamkia fursa zinazoambatana na huduma mbalimbali za msingi zinazotakiwa kuwezesha maisha ya kawaida.

Aidha, alisema kwamba katika mkutano wa uwekezaji Tanga hivi karibuni uliowezeshwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), pamoja na pato la serikali wananchi wa Tanzania sasa wajikite katika kuhakikisha kwamba wenye mradi huo wanapata mahitaji yote kutoka kwao.

Alisema pamoja na kuwepo na faida zaidi ya 11 ya mradi huo ikiwamo kuongezeka kwa mapato ya serikali kwa takribani Dola za Marekani 12.2 kwa kila pipa la mafuta ghafi litakalosafirishwa kupitia Bandari ya Tanga kulingana na kiwango cha hisa za serikali, pia uzoefu wa Watanzania utaimarika katika kushiriki masuala ya majadiliano, ujenzi na uendeshaji wa miradi ya bomba za kusafirishia mafuta.

Faida nyingine za mradi huo uliosababishwa na kugundulika kwa mafuta nchini Uganda na haja ya kusafirisha kwa gharama nafuu na salama ni kutumika kwa mkuza wa bomba kujenga miundombinu mingine, kama bomba la kusafirisha gesi asilia.

Aidha, ni matarajio ya Watanzania kwamba kutakuwepo na ongezeko la uwekezaji wa nje na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania ambao takribani watu 10,000 wataajiriwa wakati wa ujenzi na ajira zipatazo 1,000 wakati wa uendeshaji wa mradi.