Meja Jenerali mstaafu apigwarisasi Dar, Rais Magufuli amjulia hali

RAIS John Magufuli ametembelea Hospitali Kuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo jijini Dar es Salaam na kumjulia hali Meja Jenerali mstaafu Vincent Mritaba aliyelazwa hospitalini hapo baada ya kushambuliwa na watu wenye silaha wakati akiingia nyumbani kwake Ununio, Kinondoni jijini humo.

Meja Jenerali mstaafu Mritaba alishambuliwa kwa risasi juzi, na kisha kukimbizwa katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo kwa matibabu. Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Mkuu wa Kituo cha tiba cha hospitali hiyo na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, Brigedia Jenerali Paul Massawe alimueleza Rais Magufuli kuwa Meja Jenerali mstaafu Mritaba anaendelea vizuri baada ya madaktari kutoa risasi alizopigwa mkononi, kiunoni na tumboni.

Meja Jenerali mstaafu Mritaba alimshukuru Rais Magufuli kwa kumjulia hali na kumwombea dua ili apone haraka. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, pia ametembelea wodi ya majeruhi na kuwajulia hali wagonjwa wanaotibiwa katika wodi hiyo na baadaye akawasalimu wananchi waliofika hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu.

Dk Magufuli aliwapongeza madaktari wa Hospitali ya Jeshi Lugalo kwa huduma za matibabu wanazotoa kwa askari na wananchi wengine na amewahakikishia kuwa serikali itaendelea kufanyia kazi changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.

Juhudi za kupata taarifa ya shambulio hilo kutoka kwa Jeshi la Polisi hazikuzaa matunda jana, kwani Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Muliro alieleza kuwa taarifa hizo amekwisha kumpatia Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa, ambaye hata hivyo naye alisema suala hilo aulizwe Kamanda Muliro.