Mmiliki viwanda aahidi kununua pamba yote nchini

MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Namera Group of Industries, Hamza Pardesi ameahidi kununua pamba yote itakayozalishwa nchini kuanzia msimu ujao.

Hatua hii itasaidia kwa kiasi kikubwa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2015. Pardesi ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay Dar es Salaam jana, ambaye alisema tayari serikali imeanza kuwahamasisha wakulima kuongeza uzalishaji kwa kuwa kuna soko la uhakika.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa alimpongeza Pardesi kwa kuiunga mkono serikali katika mpango wake wa kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda. Kampuni ya Namera Group of Industries inamiliki kiwanda cha nguo cha NIDA na cha Namera vya Dar es Salaam.

Inatarajia kufungua kiwanda kingine cha nguo Kahama. Pia Waziri Mkuu alisema katika kuhakikisha zao la pamba linapewa kipaumbele, alikutana na wakuu wa mikoa yote inayolima pamba Septemba 8, mwaka huu na aliwaagiza wasimamie zao hilo kwa karibu ili kuinua uzalishaji wake na kuwaongezea kipato wananchi hususan wakulima wa zao la pamba.

Alisema serikali imeamua kufufua mazao makuu matano ya biashara ambayo ni pamba, chai, kahawa, korosho na tumbaku ili kuwawezesha wakulima kupata tija na kuondokana na umasikini wa kipato, hivyo kukuza uchumi wa Taifa.

Waziri Mkuu alisema serikali imeamua kusimamia kilimo cha pamba kuanzia maandalizi ya shamba, kupanda, matumizi ya pembejeo na dawa, kuvuna na kutafuta masoko, hivyo ahadi yao ya kununua pamba yote ni faraja kwa wakulima.

“Nimefurahishwa na uamuzi wenu wa kutaka kununua pamba yote itakayozalishwa nchini kuanzia msimu ujao kwani kwetu sisi ni faraja kwa sababu wakulima walipunguza uzalishaji baada ya kukosa soko la uhakika.”

Kwa upande wake, Pardesi alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba kampuni yao ina uwezo wa kununua pamba yote inayozalishwa nchini na kuichakata katika viwanda vyao na kutengeneza nguo zitakazouzwa nchini kwa bei nafuu.

Alisema kwa sasa wameajiri mafundi katika viwanda vyao ambao watakuwa wanashona nguo na kuziuza nchini kwa gharama nafuu ili kuwawezesha wananchi wa hali ya chini kumudu kununua na kuondokana matumizi ya nguo za mitumba.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo alisema kitendo cha kununua pamba inayolimwa nchini na kuchakata katika viwanda vyao kwa lengo la kutengeneza nguo za aina mbalimbali wataiwezesha serikali kuokoa fedha nyingi za kigeni zilizokuwa zinatumika kuagiza nguo nje ya nchi.