JWTZ yaonya wanaotoa, kupokea rushwa kwa ajira

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza vita dhidi ya watu wote wanaotumia jina la chombo hicho cha ulinzi ama kutoa rushwa kwa lengo la kujipatia ajira au kupokea kwa nia ya kudanganya kutoa ajira za jeshi hilo.

Hivyo, limewataka wananchi wote wanaotafuta ajira za JWTZ, kuhakikisha wanafuata taratibu zilizowekwa badala ya kutumia njia za mkato za rushwa ili kujipatia nafasi hizo. Pamoja na hayo, jeshi hilo limewahakikishia watanzania kuwa linafanyia kazi matukio yote yaliyotokea hivi karibuni yanayohusisha wananchi kupigwa risasi na kujeruhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo alisema watu wote wanaotumia njia hizo za mkato, wako hatarini kushtakiwa kwa kutafuta ajira kwa njia za rushwa. Alifafanua kuwa kuna matapeli wanaojipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kuwaahidi ajira za jeshini baadhi ya wananchi, na pindi wananchi hao wanapokosa nafasi hizo za kazi, huwasilisha malalamiko yao dhidi ya jeshi hilo.

Alisema JWTZ haitafuti wala kutangaza ajira zake kupitia mitandao ya kijamii wala kutoza fedha kwa ajili ya kutoa ajira hizo. Alifafanua taratibu za kupata ajira katika jeshi hilo kuwa ni pamoja na kupatiwa kwanza mafunzo kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) au kutoa ajira kwa wale waliotimiza vigezo kutokana na taaluma zao kama vile madaktari, wahandisi na wanasheria.

Jenerali Mabeyo alisema JKT hutangaza nafasi za kazi kupitia vyombo vya habari vinavyotambulika lakini pia hutumia halmashauri za wilaya na manispaa kuchagua wale wanaotaka kupatiwa mafunzo ya kijeshi, utaratibu unaohusisha mamlaka za mikoa. Alisema tayari jeshi hilo, limewabaini baadhi ya watu wanaojihusisha katika biashara hiyo haramu na kusisitiza kuwa hivi karibuni hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.