Mattaka atupwa jela miaka sita

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka (66) amepelekwa kwenye gereza la Ukonga baada ya kushindwa kulipa faini ya Sh milioni 35 kutokana na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kutiwa hatiani kwa mashitaka sita ikiwemo kusababisha hasara kwa shirika hiyo.

Pamoja naye, Kaimu Ofisa Mkuu, Kitengo cha Fedha, Elisaph Mathew ambaye pia alihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka sita au kulipa faini ya Sh milioni 35 kama cha mkurugenzi huyo, alilipa fedha hizo na kuachiwa huru jana. Aidha, mahakama hiyo imewataka kugawana hasara waliyoisababisha ambayo ni dola za Marekani 143,442.75 na kuilipa kwa kipindi cha mwezi mmoja, huku Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani, William Haji aliyekuwa mshitakiwa wa tatu katika kesi hiyo, aliachiwa huru baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha kosa dhidi yake.

Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa alisema mahakama imezingatia kigezo cha washitakiwa kuwa wakosaji wa kwanza na kwamba taratibu za utoaji wa adhabu zimeelekezwa na Mahakama Kuu ya kulipa faini au kifungo. Nongwa alisema upande wa mashitaka umethibitisha mashitaka hayo bila kuacha shaka yoyote baada ya kuleta mashahidi 14 kwa ajili ya kuthibitisha mashitaka hayo.

Alieleza kuwa katika mashitaka ya kwanza washitakiwa watatakiwa kulipa kila mmoja faini ya Sh milioni tano au kifungo cha miaka mitatu huku katika mashitaka ya kutumia madaraka vibaya, wametakiwa kulipa faini ya Sh milioni tano kila moja na kosa la sita la kutumia madaraka vibaya, walipe Sh milioni 10 au kifungo cha miaka sita. Alisisitiza kuwa ni dhahiri washitakiwa hao walikula njama kutumia vibaya madaraka yao na kwamba mashahidi kutoka benki waliwataja kuwa wanawatambua katika masuala ya mikopo ya manunuzi ya magari 26.