Mhasibu TRA kortini kwa hasara ya bil 29/-

WATU watatu akiwemo Mhasibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Reuben Mwakasa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi kwa kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 29.

Mbali na Mwakasa ambaye ni mkazi wa Msagara wilayani Moshi Mkoa wa Kilimanjaro, wengine ni Meneja wa Tema Enterprises, Ephraim Magete, mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam na mfanyabiashara Elizabeth Massawe, naye mkazi wa Makongo Juu jijini Dar es Salaam.

Akiwasomea mashitaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage kuwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo, kati ya Novemba 22, 2013 na Agosti 21, mwaka huu, katika maeneo mbalimbali wilaya za Temeke na Ilala, Dar es Salaam.

Nchimbi alidai washitakiwa hao kwa pamoja kwa vitendo vyao waliisababishia TRA hasara ya kiasi Sh bilioni 29 kwa kukwepa kulipa kodi kwenye mamlaka hiyo. Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Nchimbi alidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa. Hakimu Mwijage aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa walipelekwa rumande.