RC: Umeme wa nguvu ya maji kuvutia wawekezaji

MKOA wa Pwani umetangaza kuwa utatumia vyema fursa ya ujenzi wa mradi wa kuzalishia umeme wa nguvu ya maji wa Stiegler’s Gorge unaojengwa katika mto Rufi ji katika eneo la Selous kuvutia uwekezaji wa viwanda vikubwa katika wilaya za Rufi ji, Kibiti na Kisarawe.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo wakati alipotembelea eneo la Stiegler’s Gorge kukagua eneo pamoja na kuwaelimisha wananchi wa vijiji vinavyopakana na eneo hilo faida ambazo watazipata kupitia mradi huo.

Aliongozana na maofisa waandamizi wa mkoa huo kukagua mto Rufiji eneo la mradi ambao Serikali ya Awamu ya Tano imetangaza kujenga mradi mkubwa wa umeme utakaozalisha megawati 2,100 kwa ajili ya kuondoa tatizo la umeme nchini.

Akizungumza baada ya kutembelea eneo hilo, Ndikilo amewahakikishia wakazi wa Rufiji kwamba ujenzi wa mradi huo utakuwa kivutio kikubwa cha uwekezaji wa viwanda katika wilaya za Rufiji, Kibiti na Mkuranga.

Alisema ujenzi wa mradi huo pia utapunguza kabisa tatizo la mafuriko lililokuwa likiikumba Wilaya ya Rufiji pamoja na kuwezesha wakazi wa wilaya hiyo kujikita zaidi katika kilimo cha umwagiliaji.