Ubungo watakiwa kufuatilia fedha za miradi

WANANCHI wameombwa kuwa na utaratibu wa ufuatiliaji rasilimali fedha zinazotengwa katika kata zao kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kusaidia utekelezwaji wa utoaji huduma za kijamii.

Akizungumza wakati wa ufungaji wa semina ya siku tatu ya mafunzo kwa wananchi juu ya ufuatiliaji wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maji katika kata tatu za halmashauri ya Ubungo, diwani wa kata ya Kibamba, Ernest Mgawe alisema wananchi wana haki ya kufuatilia fedha za miradi ya maji zinazotengwa na serikali kuu ili kujiletea maendeleo.

Semina hiyo iliyoandaliwa na Pakacha Group kwa ufadhili wa taasisi ya ‘The Foundation for Civil Society ‘kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wananchi kufuatilia fedha zinazotengwa kwa ajili ya utoaji wa huduma wa maji katika kata tatu za Kwembe, Kibamba na Msigani.

Diwani Mgawe alisema wananchi wanaweza kufanya ufuatiliaji kupitia mfumo wa Usimamizi na ufuatiliaji wa Rasilimali za Umma (Pets) ukiwa na malengo ya kuboresha huduma za kijamii, kuhakiki utendaji wa serikali za mitaa na kuwezesha uandaaji wa mipango shirikishi.

Pets ni mfumo unaowezesha ufuatiliaji matumizi ya rasilimali za umma zinazotoka serikali kuu au halmashauri kwa maendeleo ya wananchi kuanzia ngazi za mitaa hadi kata na kuendelea.

Aidha Diwani huyo alisema kuwa kamati za maji za mitaa na kata zinawajibu wa kushirikiana katika kutatua changamoto za maji, ambayo ni muhimu katika mahitaji ya kila siku. “Wananchi wenye shida ya maji katika mitaa yao wajiorodheshe, wakishirikiana na madiwani wao na watendaji ili kuhakikisha kata zetu zinafikiwa na maji,” alisema diwani huyo.

Akizungumza katika semina hiyo ya siku tatu, mkuu wa kitengo cha matengenezo idara ya maji manispaa ya Ubungo, Josephat Rwilemera alisema semina hiyo ni muhimu kwa wananchi wa kata hizo ili kuhakikisha wanashirikiana na Dawasco katika utekelezaji wa miradi ya Maji.

“Maji yanapatikana kwa asilimia takriban 70 katika kata za Halmashauri za Ubungo na jitihada zinaendelea kuhakikisha huduma hiyo inafikiwa na watu wengi kupitia mradi unaofadhiliwa na serikali ya India chini ya ujenzi wa Wachina,” alisema Rwilemera.

Akizungumza katika semina hiyo, mmoja wa wananchi wa kata ya Msigani, Halima Isaya alisema kuwa kata yake haina huduma ya maji, hivyo mafunzo ya Pets aliyoyapata yamemjenga ili kufuata taratibu zinazotakiwa katika ufuatiliaji Wa miradi ya maji katika kata yake.