Magufuli aiweka tanzanite kwenye himaya ya JWTZ

RAIS John Magufuli ameagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na Shirika la Uchumi la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT), kuanza mara moja kujenga uzio kwenye eneo la kitalu A hadi D lililopo eneo la Mererani, Simanjiro, ambalo kunapatikana madini ya kipekee ya tanzanite.

Aidha, ameagiza kufungwa kwa kamera maalumu, kuweka uzio maalumu na kutakuwa na eneo moja la mlango wa kutokea na kuingia ili kubaini wezi wanaoiba madini hayo. Rais Magufuli alisema hayo jana eneo la Naisinyai lililopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara wakati alipozindua barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 26 kutoka Kia/ Mererani, iliyojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 32.5 ambazo ni fedha zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.

Alisema sababu kubwa ya kuamua kujengwa kwa uzio huo na kufungwa vifaa maalumu ni kudhibiti wizi wa madini hayo ya tanzanite, ambayo yanapatikana nchini Tanzania pekee, lakini hayawanufaishi Watanzania waliopo eneo hili wala serikali kupata mapato.Pia aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama, kuwaachia wawekezaji wanaoshikiliwa kutokana na suala hilo la tanzanite na kushirikiana kwa pamoja na timu ya kupitia mikataba ya madini iliyopo chini ya Profesa Palamagamba Kabudi ili kuboresha mikataba ya madini na kila mmoja anufaike na madini hayo, ikiwemo wananchi wanaozunguka maeneo ya migodiyote ya madini.

Alisema ni vyema sasa soko la tanzanite au mnada wa madini hayo, kufanyika Simanjiro yanapochimbwa madini hayo na si mnada huo kufanyika jijini Arusha. Alisisitiza kuwa lengo la soko hilo, kufanyika Simanjiro ni kufungua fursa za biashara kwa wananchi, wachimbaji wadogo wa tanzanite na madini mengine yanayotoka eneo hilo. Alisema eneo la tanzanite lina ukubwa wa kilometa 81.99 za mraba, ambalo lipo Kitalu A hadi Kitalu D na kilometa za mraba 13 zilizobaki ni namba moja hadi nne, ambazo ni za wachimbaji wadogo.

Alisema tanzanite imeibwa sana na watu walifanya kama shamba la bibi na kusisitiza kuwa viongozi wanapopewa mamlaka ya kusimamia rasilimali za Taifa ni vyema wakazisimamia kwani Tanzania si nchi masikini, bali umasikini unaletwa na watu wachache. “Katika uongozi wangu sitakubali kuibiwa na nitasimamia mali za wananchi ziwe salama. Haiwezekani unapopambana na jambo fulani yanaibuka mambo mengine ambayo yanataka kukwamisha jambo unalolisimamia. Nasema hivi sitakubali kuona rasilimali za nchi hii zinachukuliwa na wengine, hebu oneni mna madini haya, lakini hamna hata gari la wagonjwa inasikitisha,” alieleza Dk Magufuli.

Alisema endapo tanzanite hiyo ingekuwa nchi nyingine, eneo la Simanjiro lingekuwa kama Ulaya, lakini kwa mujibu wa ripoti iliyoundwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania, Job Ndugai, madini hayo hayawanufaishi Watanzania wala wananchi wa eneo hili la Simanjiro. Alisema asilimia tano tu ya madini ndiyo Tanzania inapata faida na inayobaki yote ni faida kwa wawekezaji na wezi, lakini endapo yangetumiwa vyema, kusingekuwa na matatizo ya kero ya barabara, gari la wagonjwa, kero ya maji, na cha kushangaza kabisa wachimbaji wa madini hayo hawana uhuru wa kununua au kuuza madini haya.

Akizungumza kuhusu uzinduzi wa barabara hiyo, Rais Magufuli aliwapongeza wananchi wa Tanzania kwa kulipa kodi, zilizowezesha wananchi wa eneo hilo la Simanjiro kupata barabara ya lami tangu kupata uhuru. Alisema lengo la barabara hiyo kuwekwa lami ni kufungua milango ya biashara pamoja na kupunguza kero ya usafiri waliokuwa wakiipata wananchi hao. Alisema barabara hiyo itawezesha kuunganisha mawasiliano baina ya mikoa mbalimbali nchini.

Baadhi ya wabunge waliofika kushuhudia uzinduzi huo, Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM), James ole Millya ambaye ni Mbunge wa Simanjiro (Chadema), walimpongeza Rais Magufuli kwa jitihada zake za kuhakikisha anatatua changamoto mbalimbali za wananchi. Ole Millya alisema wananchi wa jimbo lake, wanashukuru kwa ujio wa barabara hiyo tangu nchi kupata Uhuru, lakini wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa gari la wagonjwa pamoja na kero ya maji, hivyo wanamuomba Rais Magufuli kuwasaidia kuzitatua.