Mmarekani ashinda kesi ya mirathi ya baba yake

JAJI Salma Maghimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha juzi alimpa mamlaka Carren Kindondechi, kusimamia mirathi ya baba yake, Alfred Leo aliyekuwa akimiliki mali yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 50 jijini Arusha.

Hata hivyo, uamuzi huo wa Kindondechi ambaye ni raia wa Marekani na mtoto wa marehemu Leo kusimamia mali hizo, umepingwa na watoto wengine wawili wa marehemu, Conrad Leo na Allan Leo wanaoishi nchini kwa madai kuwa Kindondechi na kaka yake, Kelvin Leo hawatambuliki katika ukoo wa Leo na kisheria hawapaswi kusimamia mali hizo. Kabla ya uamuzi wa juzi wa Jaji Maghimbi, kesi hiyo iliwahi kufunguliwa na Kelvin ambaye ni kaka ya Carren kupitia kwa wakili Salim Mushi wa Kampuni ya Uwakili ya Elite, Juni 24, 2015 na kusikilizwa na Jaji Fatuma Massengi ambaye aliitupilia mbali kwa maelezo kuwa Kelvin hawezi kusimamia mirathi hiyo kwa kuwa hana sifa za kisheria kuwa msimamizi wa mirathi hiyo.

Kesi hiyo ilirudishwa katika mahakama hiyo, na Jaji Maghimbi katika uamuzi wake, alisema Kindondechi ana sifa za kusimamia mirathi ya marehemu baba yake na sheria inaeleza hivyo kuwa mtoto huyo anaruhusiwa kisheria kusimamia mirathi. Kutokana na uamuzi huo, Allan na Conrad wamesema watakata rufaa Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu ya Jaji Maghimbi kwa madai kuwa mahakama moja haiwezi kuwa na maamuzi mawili tofauti na kuitaka Mahakama ya Rufaa kutengua hukumu hiyo.

Allan alisema mbali ya kukata rufaa ngazi ya juu kutaka kupata ufafanuzi wa kisheria juu ya jambo hilo, pia wametoa taarifa ya kusitisha uuzwaji, ukusanyaji kodi wa nyumba za marehemu baba yao na uendeshaji wa shughuli zote za kibiashara. Awali aliyekuwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo ya Maromboso, Simaitoni Joseph katika uamuzi wake Januari 27, mwaka juu alisema usimamizi wa mirathi unapaswa kushirikisha watoto wa hapa nchini na wa nje na siyo wa upande mmoja.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo mahakamani hapo, mali alizoacha marehemu ni magari zaidi 18 ya aina mbalimbali, viwanja vitano vilivyoko Moshono na Sakina, nyumba tisa na za kisasa zilizopo eneo la Uzunguni na Sakina, hoteli ya kitalii ya Lion na hisa za kampuni ya Lion International, vyote vinadaiwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh bilioni 50.