Bosi IPTL awasilisha ombi la dhamana Mahakama Mafisadi

MMILIKI wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Power African Power (T) Limited (PAP), Habinder Sigh Sethi amewasilisha maombi ya dhamana katika Mahakama Kuu, kitengo cha makosa ya rushwa na uhujumu uchumi inayojulikana kwa jina la Mahakama ya mafi sadi.

Sethi ambaye anawakilishwa na Wakili Joseph Makandege, aliwasilisha maombi hayo namba 29, 2017 mbele ya Jaji Winfrida Koroso. Hata hivyo, Jaji Koroso amepanga Septemba 26, mwaka huu kuanza kusikiliza maombi hayo. Kwa mujibu wa Makandege, anaomba mteja wake apatiwe dhamana katika kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Katika hati ya kiapo alidai kuwa Juni 16, mwaka huu, alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akielekea Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu. Alidai kuwa siku hiyo alivyokamatwa alifunikwa uso na kushambuliwa na kupelekwa sehemu isiyojulikana na watu wenye silaha. Alidai Juni 19, mwaka huu mshitakiwa aliwekwa kituo kikuu cha polisi na baadaye alipelekwa mahakamani siku hiyo hiyo na mtu mwingine ambaye ni James Rugemarila wakikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi ambayo ni kula njama, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kujipatia fedha kwa njia ya udanganjifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara.

“Julai 3, mwaka huu kabla ya kuomba dhamana upande wa mashitaka ulifanya mabadiliko kwenye hati ya mashitaka na kuongeza mashitaka sita ya utakatishaji fedha hivyo kufanya jumla ya mashitaka 12,” alidai Makandege. Wakili Makandege alidai anaamini kuwa makosa ya utakatishaji fedha hayana dhamana lakini katika mazingira kadhaa mahakama inaweza kuchepuka katika msimamo huo na kutoa dhamana.

Aliendelea kudai baadhi ya mazingira hayo ni pamoja na Sethi kuwa mgonjwa na kuhitaji uangalizi wa wataalamu bila hivyo kuna uwezekano wa kupoteza maisha na kushindwa kuendelea na mashitaka yanayomkabili. Pia katika hati ya kiapo alidai alifanyiwa upasuaji Afrika kusini mara mbili na mwaka huu mara moja ambapo aliwekewa puto tumboni mwake na hivyo anahitaji kuwa na mtaalamu wa kumuangalia mara kwa mara.