Majonzi, vilio vyatawala 5 familia ya Teu wakizikwa

MJI wa Mpwapwa mkoani Dodoma na viunga vyake jana ulitawaliwa na vilio, majonzi na simanzi wakati miili ya watu watano kati ya sita wa familia ya Gregory Teu iliyotakiwa kuzikwa, ikilazwa kwenye nyumba ya milele.

Licha ya kuchimba makaburi sita kwa ajili ya maziko ya watu hao sita kati ya 13 waliokufa katika ajali ya gari Jumapili wiki hii nchini Uganda, kaburi moja halijawekwa mwili wa marehemu baada ya mwili wa Esther Teu kubakizwa ili kuzikwa Dar es Salaam ambako alikuwa ameolewa. Wote hao ni wana familia wa aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na baadaye Viwanda na Biashara katika Serikali ya Awamu ya Nne, Gregory Teu ambao walikufa kutokana na gari aina ya Toyota Coaster kugongana na lori nje kidogo ya Kampala wakiwa njiani kurejea nchini baada ya kuhudhuria harusi ya binti wa Teu, Dk Annette Teu na mumewe, Dk Treauseur Ibingira wa Uganda.

Wote ni madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza. Waliozikwa katika makaburi ya Viwanja vya Kanisa Kuu la Watakatifu Wote la Kanisa la Anglikana Mpwapwa ni George Teu (baba wa Gregory), baba yake mdogo Alfred Teu, shangazi yake Paulina Ndagala, dada yake Rehema Teu na mwanawe wa kwanza, Sakazi Teu isipokuwa Ester aliyezikiwa Dar es Salaam.

Mazishi hayo yaliyotanguliwa na Ibada ya Misa iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Anglikana Tanzania na Askofu wa Dayosisi ya Mpwapwa Watakatifu Wote, Jacob Chimeledya akisaidiwa na Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo Anglikana Tanzania, Donald Mtetemela na mazishi yaliongozwa na Askofu mstaafu, Dk Simon Chiwanga. Chimeledya alisema haijawahi kutokea katika kanisa hilo na Mpwapwa kwa ujumla kupata misiba mingi namna hiyo, ya familia moja, ni jambo limeleta simanzi ya kutosha katika mji huo.

Akihubiria umati uliofurika kanisani na nje ya kanisa, Askofu Chimeledya alisema kifo ni fumbo kubwa lipo kati yetu na tulipokee katika maisha ya kila siku tukilinganisha na yaliyompata Ayubu. Ayubu alipata mapigo ya kufiwa na wanaye, mifugo, ngamia na watumishi wake, hivyo hakuna anayeweza kutambua wala kujua siku ya kifo chake. “Kila binadamu anatakiwa kujiandaa kutoka na kwamba hakuna ajuaye siku ya kifo chake,” alisema askofu huyo, na kuwataka waumini mamia waliofurika ndani na nje ya kanisa hilo hadi makaburini, kwamba kila mtu afanye vizuri na wajifunze kuhesabu siku zao kwani hawajui siku wala saa ya kifo chao.

Akizungumza Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema msiba huo ni jambo gumu, ni vigumu kulizoea, “afe mtoto hazoeleki au mtu mzima inahuzunisha pia.” Ndugai alisema kilichotokea ni mpango ya Mungu kama ilivyotokea kwa Ayubu kama jina lake yeye (Job) na hiyo ni kazi ya Mungu haina makosa, bali kutakiwa kuipokea. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema mkoa unaungana na salamu za Rais John Magufuli na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kuwaombea wana familia kwa msiba mzito uliowapata.

Akizungumza Kiongozi wa Ujumbe wa Serikali, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Suzan Kolimba aliipongeza Serikali ya Uganda kwa kugharamia usafirishaji wa miili ya marehemu 13 hadi Dar es Salaam, pamoja na kugharamia matibabu ya majeruhi waliobaki hospitalini. “Tunampongeza Rais Museveni kwa kusimamia kwa karibu suala la msiba tangu Septemba 18, mwaka huu walipopata ajali katika Mji wa Kampala.

Rais Magufuli aliagiza wizara ya mambo ya nje ya Tanzania kuhakikisha inarejesha miili hiyo lakini kazi hiyo imekuwa nyepesi kutokana na serikali ya Uganda kutoa msaada huo,” alisema. Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje alisema wanaishukuru Serikali ya Uganda kwa kusaidia kusafirisha miili ya marehemu watano kutoka Dar es Salaam. “Tumshukuru Mungu, kwani kila binadamu atakufa na hatujui tutaondokaje lini, tupokee msiba ni wetu,” alisema Lubeleje, huku Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene akiomba Mungu awasaidie katika kulichukua jambo hilo gumu.

Akizungumza Mzee wa Kanisa la Watakatifu Wote, George Mbuti alisema kabla ya kutokea ajali hiyo, mwezi mmoja uliopita, Mzee Alfred Teu alifanya kitendo cha kushangaza wengi cha kukabidhi pinde kwa mtoto wake, Kenneth Temu, kama alama kuwa kiongozi wa familia ya mzee huyo. Kitendo kilishangaza wengi kwani si kawaida kwa mila za kabila la Kigogo kufanya kabla ya kufa.

Kitu cha pili, kwa kawaida mila za Kigogo anayekabidhiwa pinde ni mtoto mkubwa, lakini Alfred alikabidhi pinde kwa mtoto wa kati kati. Kitendo ambacho kilikuwa kinaonesha alijua au kutabiri kwamba siku za kuishi duniani zitafupika. Alifanya hivyo, kwa madai mtoto wake mkubwa alikuwa hampendi mzazi huyo na baba alikuwa hana upendo kwa mtoto huyo, Girbeeth, ambaye alikuwa akimtuhumu kuwafanyia mambo ya kishirikina nyumba yao ambayo ndiyo kubwa ya kwanza katika nyumba za mzee huyo. Licha ya kutoa pinde hiyo kwa mtoto mdogo, kabla hajafariki dunia, kwa mila za Kigogo itabaki hivyo hivyo,