Ajali yaua kondakta, yajeruhi sita

KONDAKTA wa basi la kampuni ya Kidia One, Malisa Heavson amekufa na watu sita kujeruhiwa baada ya basi hilo kupata ajali katika eneo la kijiji cha Samuye wilayani Shinyanga kwenye barabara kuu iendayo Dar es Salaam.

Kaimu Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga, Lutusyo Mwakisya alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana, majira ya saa tano na kueleza kuwa basi hilo lenye namba za usajili T964 CCQ aina ya Yutoung lilikuwa likitokea mkoani Mara likiendeshwa na dereva Abdul Nyasaka. Alisema chanzo cha ajali hiyo ni kutokana na dereva kujaribu kukwepa ng’ombe na kupinduka na kusababisha kifo cha kondakta wa basi hilo Heavson na abiria sita kujeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao.

Alisema baada ya kutokea kwa ajali hiyo dereva alikimbia kusikojulikana hivyo polisi inaendelea kumtafuta kwa mahojiano zaidi. Aliwataja majeruhi kuwa ni Wang Xiang (25), Lucas Peter 23, Oliver Evarist (22), Remmits Cosmas (39) Bazila Mushi (26) , Jiang Baiwu (36) na kuongeza kuwa raia wa China, mwenye makazi yake nchini Kenya, Wang Xiang aliyevunjika mkono na hali yake kutokuwa nzuri alikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando iliyopo jijini Mwanza.