TCRA yazindua kampeni kudhibiti maudhui yasiyofaa

WAKATI Mamlaka ya ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezindua kampeni ya matumizi salama na sahihi ya mitandao ya kijamii, Jeshi la Polisi limebainisha kuwa uhalifu wa mtandao unaoongoza hasa utumaji na usambazaji wa taarifa za uongo.

Kampeni hiyo ya ‘Usinitumie, Sitaki, Situmii wengine, nitakuripoti,” imezinduliwa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Bodi ya TCRA, Dk Jones Kilembe ikiwa na lengo la kusisitiza matumizi salama na sahihi ya mitandao kwa umma. Kabla ya uzinduzi huo, uliokwenda na warsha juu ya matumizi bora ya habari mtandaoni, iliyoshirikisha wamiliki wa mitandao ya kijamii (bloga), Dk Kilembe alibainisha kuwa kutokana na ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano, matumizi ya mitandao imeongezeka, jambo ambalo limevutia wasio na taalumu ya habari na wale wenye taaluma na kuleta changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na kutofuata maadili.

“Kwa sasa tuna zaidi ya televisheni za mtandaoni 50, zaidi ya blogu 150 na maendeleo ya teknolojia na kuanza matumizi ya simu za kisasa imechangia udhibiti wa maudhui kuwa mgumu, jambo ambalo limeifanya TCRA kusisitiza ufuatiliaji wa karibu kwa maendeleo ya nchi kijamii, uchumi na siasa,” alisema.

Akizungumzia hali ya usalama mitandaoni, Ofi sa wa Jeshi la Polisi kutoka Kitengo cha Makosa ya Mtandao, Joshua Mwangasa alibainisha kuwa pamoja na kuwa mfumo wa mtandao wa Tanzania kuwa salama ukilinganisha na nchi zingine za Afrika, lakini kwa sasa uhalifu wa kutuma na kusambaza taarifa za uongo umekuwa ukisumbua.

Aidha, alisema uhalifu wa mtandaoni umekuwa ikipungua kati ya mwaka 2015 hadi 2017 huku kesi zilizoripotiwa polisi zikiwa 5,172 kwa mwaka 2015 na makosa yaliyoripotiwa kwa mwaka 2017 hadi Juni ni kesi 3,346.

“Jeshi la polisi limekuwa likifanya doria kwenye mtandao, lakini hii haimaanishi tunaingilia faragha za watu, bali tunafanya doria kwenye mitandao ya wazi ambayo inashirikisha umma, hivyo watu waache kutumia vibaya tekinolojia hii,” alisema na kuongeza kuwa jambo la msingi ni kutoa elimu kwa umma na matumizi salama na sahihi ya mitandao na kwamba kwa kufanya hivyo, uhalifu wa mitandaoni utapungua kwa asilimi 90.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Valerie Msoka alipongeza baadhi ya mitandao ya kijamii kwa kazi nzuri wanayofanya na kusisitiza kuwa kamati yake itaendelea kutoa elimu kwa umma.