BoT yaingilia kati sakata pesa za Lissu

WAKATI Ofi si ya Bunge ikisisitiza kuwa fedha zilizochangwa na wabunge kiasi cha Sh milioni 43 kwa ajili ya kusaidia matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), tayari zimetumwa katika akaunti ya Hospitali ya Nairobi nchini Kenya anakopatiwa matibabu, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeingilia kati.

Kwa sasa Lissu anaendelea na matibabu nchini Kenya baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana mkoani Dodoma, Septemba 7, mwaka huu.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari, Elimu kwa Umma na Mawasiliano cha Bunge kwa vyombo vya habari jana, fedha hizo zimetumwa kupitia BoT.

Taarifa hiyo ilisema kwa mujibu wa viwango vya kubadilishia fedha vya BoT kwa siku hiyo wakati fedha hizo zikitumwa ilikuwa ni sawa na Shilingi za Kenya 1,977,120.58. Ofisi ya Bunge imeeleza kuwa kiasi hicho cha fedha kilitumwa siku ya Septemba 20, mwaka huu kwenda Benki ya Barclays, tawi la Hurlringham, kwenye akaunti namba 0451155318 yenye jina la Kenya Hospital Association.

Taarifa hiyo iliambatanisha barua yenye kumbukumbu, Ref.NO FA.93/155/01B/260 kutoka kwa Meneja wa Akaunti za Nje wa BoT inayothibitisha benki hiyo kutuma fedha hizo kwa akaunti hiyo ya hospitali anakotibiwa Lissu. Ofisi hiyo ya Bunge imelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe alipozungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, kulitupia lawama Bunge na hasa akielekeza tuhuma zake kwa Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai kuwa wabunge wamekatwa posho kuchangia gharama za matibabu ya Lissu, lakini fedha zilizopatikana hazikuwa zimekabidhiwa.

Hata hivyo, Spika Ndugai alimjibu Mbowe na kumtaka aache kupotosha taarifa za ushiriki wa Bunge katika tiba ya Lissu na kulichukuliwa suala hilo kisiasa. Alifafanua kuwa ni utaratibu wa kawaida kwa Bunge au ofisi inayotumia bima, iwapo inataka mgonjwa wake kuhamishiwa hospitali nyingine, lazima itoe taarifa ya daktari inayoelezea kuhamishwa kwa mgonjwa huyo.

Aidha, Ndugai alimtaka Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni kukubali ofa ya serikali ya kutaka kugharamia tiba za Lissu akiwa nje ya nchi. Kwa sasa matibabu ya Lissu yanatokana na michango ya wadau mbalimbali ambapo kwa mujibu wa Mbowe hadi juzi jumla ya Sh milioni 204 zilikusanywa ambazo hata hivyo alibainisha kuwa hazitoshi na michango inaendelea. Kwa mujibu wa msemaji wa familia ya Lissu, Alute Mughwai, hali ya mbunge huyo inaendelea kuimarika na kwamba aliweza kuzungumza naye kwa kutumia simu ya kiganjani na kuwashukuru Watanzania kwa sala na michango yao.