TSN yapania kukivusha Kiswahili EAC

KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali (TSN), imepania kuwa daraja la kukivusha Kiswahili kuelekea kuwa lugha rasmi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

HabariLEO –Toleo la Afrika Mashariki- ndilo gazeti la kwanza la Kiswahili linalochapishwa na kuuzwa katika nchi sita wanachama wa EAC ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. Dhamira ya TSN inayochapisha gazeti hili pamoja na Daily News, Sunday News na SpotiLEO, ilielezwa jana na Mhariri Mtendaji wake, Dk Jim Yonazi alipokutana na kuzungumza na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAKC), Profesa Kenneth Simala katika ofisi za kamisheni hiyo mjini Zanzibar.

Dk Yonazi alisema kupitia gazeti lake la HabariLeo, imenuia kukuza na kueneza Lugha ya Kiswahili katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, na ndiyo maana imeanza kuchapisha toleo maalumu kwa ajili ya wasomaji wa nchi za EAC linalotoka kila Jumanne sanjali na Daily News ambalo huchapishwa kwa lugha ya Kiingereza. “Nimemueleza kwamba TSN ina nia ya kuwa na ushirikiano na Kamisheni hiyo kwa faida ya jumuiya yetu. Nimemuomba kwamba tushirikiane kufikia lengo hilo,” alisema Dk Yonazi alipozungumza na gazeti hili.

Dk Yonazi pia alimkabidhi Profesa Simala picha ya toleo la kwanza la HabariLEO kwa ajili ya nchi za Afrika Mashariki ambalo kwa mara ya kwanza liliingia mtaani Agosti 21, mwaka huu. Aliongeza kuwa Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki na TSN wameafikiana kuandaa makubaliano ya ushirikiano yatakayowezesha kufanya kazi kwa pamoja katika kukuza lugha ya Kiswahili.

Ushirikiano huo utawezesha kuwa na mipango mbalimbali itakayowezesha nchi zote za Afrika Mashariki kufaidi ubora na matunda ya lugha ya Kiswahili. Naye Profesa Simala ambaye alimkabidhi Dk Yonazi kitabu cha Mpango Mkakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ameipongeza TSN kwa wazo na ubunifu wa kuwa na toleo maalumu la HabariLEO kwa ajili ya wasomaji wa Afrika Mashariki, akisema amefurahia na kulipokea wazo hilo kwa mikono miwili.

Amesifu pia uzalendo wa uongozi wa TSN katika kufikiria kuwaunganisha wananchi zaidi ya milioni 150 wa Afrika Mashariki kupitia lugha adhimu ya Kiswahili ambayo imepitishwa kuwa moja ya lugha rasmi katika nchi wanachama wa EAC. Profesa Simala alifafanua kuwa Kiswahili ni lugha rasmi ya Jumuia ya Afrika Mashariki na kwamba hata katika Mkataba wa Afrika Mashariki, Kipengele cha 137, unatilia mkazo kukuza Kiswahili kwa ajili ya mtangamano na maendeleo endelevu ya lugha hiyo.

Aliongeza kuwa kwa sasa nchi nyingi duniani zinafurahia lugha ya Kiswahili na hata kuifundisha katika ngazi mbalimbali za elimu ikiwa ni pamoja na vyuo vikuu. Baadhi ya nchi alizozitaja kuwa zimechukua hatua za makusudi kutumia Kiswahili ni pamoja na Ujerumani, Urusi, China, Korea Kusini, Japan na Marekani. Pia kuna nchi zingine ambazo hufundisha Kiswahili katika taasisi mbalimbali za elimu.

Hivi karibuni, akifunga Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Kiswahili kwa nchi za Afrika Mashariki mjini Zanzibar, Naibu Waziri Mkuu wa Uganda ambaye pia ni Waziri anayeshughulikia Masuala ya Afrika Mashariki, Kirunda Kivejinja, alisisitiza umuhimu wa kukuza lugha ya Kiswahili ili iwaunganishe kwa haraka watu zaidi ya milioni 150 wa nchi za EAC.

Kivejinja ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa EAC, alisema ni kupitia Kiswahili watu wanaweza kuunganishwa kwa haraka katika mtangamano wa jumuiya hiyo. Katika kuunga mkono hilo, wadau wa Kiswahili walioshiriki Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Kiswahili kwa nchi za Afrika Mashariki mjini Zanzibar hivi karibuni, wameshauriwa kuwa ili kuongeza kasi ya ukuaji wa lugha hiyo, nchi wanachama wa EAC zielekeze nguvu katika kufundisha Kiswahili shuleni na vyuoni, na ikiwekezekana kuwe na madarasa ya elimu ya watu wazima kwa ajili ya lugha ya Kiswahili.

Katika kongamano hilo la siku tatu lililoandaliwa na EAKC iliyopo chini ya EAC, Kivejinja alisema lugha hiyo ni maarufu duniani na ina asili ya Afrika Mashariki, hivyo kuna ulazima wa watu wake kuijua kwa kina, huku akiwasisitiza viongozi wa nchi za EAC kuhimiza matumizi ya lugha hiyo huku akiitaka EAKC kuangalia uwezekano wa kujenga hoja ili Kiswahili kitumike kurahisisha kuyafikia malengo ya jumuiya.

“Niwaombe mawaziri wanaohudhuria kongamano hili, wayafanyie kazi maazimio yake… yana uzito mkubwa katika ustawi wa lugha husika, lakini pia kwa manufaa ya nchi zetu,” alisema. Alisema Tanzania inasifika kwa umoja, mshikamano na amani kutokana na kuwa na lugha moja kuu, Kiswahili licha ya kuwa taifa kubwa lenye mtawanyiko wa makabila zaidi ya 120.

“Nawapongeza sana waasisi wa taifa la Tanzania kwa kuona umuhimu wa kuwa na lugha ya kuwaunganisha Watanzania… wamefanikiwa na leo hii Watanzania ni wamoja, hakika tunapaswa kujifunza kitu kutoka kwa Tanzania ili tuwe na jumuiya imara ya Afrika Mashariki,” alisema Kivejinja. Naye Profesa Simala aliwaeleza wajumbe kuwa, washiriki wa kongamano hilo wanafanya kazi kwa karibu na vyama vya Kiswahili Afrika Mashariki ili kuhakikisha lugha hiyo inachangamkia na kukuza ustawi wa EAC na watu wake.

Katika kongamano hilo, wadau kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na nje ya ukanda huo, walishiriki ili kuweka mikakati ya kukuza lugha ya Kiswahili kama lugha kuu ya mtangamano kwa lengo la kukuza maendeleo kwa haraka. Hivi karibuni Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (TATAKI), Dk Ernesta Mosha ilisema Kiswahili ni lugha muhimu ya mawasiliano kwa nchi za Afrika Mashariki, kwa kuwa inafundishwa katika viwango vya elimu, shughuli za kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Aliongeza kuwa, kutokana na umuhimu huo, wahadhiri wa vyuo vikuu vya ndani na nje ya Afrika Mashariki kwa sasa wapo TATAKI kujifunza lugha hiyo ngazi ya shahada za juu. Dk Mosha alisema kutumika kwa lugha hiyo kwa kiasi kikubwa kunaimarisha umoja na ushirikiano kwenye nchi wanachama EAC na pia inaendelea kuwa lugha ya ukanda huo.

Kwa mujibu wa Dk Mosha, Taasisi inaendelea kushirikiana na vyuo vikuu Afrika Mashariki na nje ya eneo hilo kuhakikisha Kiswahili kinaendelea kukua na kuenea, kupitia mikataba ya ushirikiano, tafiti za kitaaluma za pamoja, warsha, semina na makongamano ya kitaaluma kupitia vyama vya kitaaluma kikiwemo Chama cha Kiswahili cha Afrika Mashariki (Chakama) na Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (Chaukidu).