JPM ashtushwa Fuso iliyoua 15

RAIS John Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko taarifa ya vifo vya watu 15 na wengine sita kujeruhiwa baada ya gari la mizigo aina ya Fuso walilokuwa Sumbawanga kwenda Kijiji cha Wampembe mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi mkoani Rukwa, kugonga mwamba na kupinduka.

Rais alitoa kauli hiyo katika salamu alizompelekea Mkuu wa mkoa wa Rukwa Zelothe Steven jana. Ajali hiyo inasemekana kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea wilayani Nkasi. Mkuu huyo wa mkoa Zelothe Steven akifuatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda walifika eneo la ajali jana alfajiri. Lori hilo lilikuwa pia limebeba mahindi.

Mmiliki wa Fuso yenye namba za usajili T 425 BFF ni Bakari Ally Kessy ambaye ni mtoto wa kiume wa Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy kupitia CCM. Akizungumzia ajali hiyo ya barabarani, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mtanda alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa tisa alasiri na kuwa gari hilo lilikuwa likitokea Sumbawanga Mjini kwenda Kijiji cha Wapembe wilayani humo.

“Gari hilo lililokuwa na abiria 21 na shehena ya mizigo lilipofika katika eneo la mbuga nyeupe lilimshinda dereva na kugonga mwamba na kuanguka. Watu 12 walikufa papo hapo na wengine watatu wamekufa muda mfupi baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa kwa matibabu,” alieleza Mtanda.

Aliongeza kuwa dereva wa gari hilo inasemekana ilikuwa mara yake ya kwanza kupita katika barabara hiyo ambayo ina kona kali hiyo alishindwa kulimudu wakati akiteremka milima wenye kona kali na kupinduka.

Alisema dereva huyo ambaye majina yake hayakufahamika mara moja, amekimbia kusikojulikana muda mfupi baada ya kutokea kwa ajali hiyo. “Miili sita ya marehemu hao ambao majina yao hayajafahamika imehifadhiwa katika Kituo cha Afya Mvimwa ikisubiri kutambuliwa na ndugu zao,” aliongeza.

Aliongeza kuwa maiti zikitambuliwa gharama za maandalizi ya maziko na usafiri zitatolewa na serikali. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema waliokufa ni abiria 15, miongoni mwao wanawake ni 10 na wanaume ni watano pamoja na majeruhi tisa.

Waliokufa wametambuliwa kuwa ni Domona Tenganamba (41), Emmanuel Rashid (84), Restuta Sunga (35), Salula Revana (64), Felisia Tenganamba (1), Prisca Madeni (45), mwalimu wa shule Richard Chikwangara (24), Yusta Somamabuto (36), Grace Ramadhan (24), Odetha Madirisha (46), Megi Nalunguli (52), Abdul Amani (37), Nyandindi Batrahamu (35) na mtoto mwenye umri wa wiki mbili ambaye alikuwa hajapewa jina.

Majeruhi ni pamoja na Dimas Clement (26), Sema Savery (25), Allu Haruna (33), Yusta Mfundwima (50), Tenesfory Oscar (36), Amos Ktambale (25), Neema Mwanandenje (21), Joseph Sungura (28) na mwanamke mmoja ambaye majina yake hayakutambuliwa mara moja.

Rais Magufuli akizungumzia ajali hiyo alisema: “Natambua hiki ni kipindi kigumu kwa wanafamilia wote waliopoteza ndugu zao katika ajali hii, natambua kuwa wamepoteza wapendwa wao na watu muhimu waliowategemea, nawapa pole sana kwa kufiwa na naungana nao katika maombi ili roho za marehemu zipumzishwe mahali pema peponi, Amina,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia amewaombea majeruhi wote wa ajali hii wapone haraka ili warejee katika afya njema na kuungana na familia zao katika maisha yao ya kila siku. Aidha, Rais Magufuli amezitaka mamlaka zinahusika na masuala ya usalama barabarani kuongeza juhudi zitakazowezesha kukabiliana zaidi na matukio ya ajali za barabarani ili kuokoa maisha ya watu na mali.