Polisi yatibua utapeli wa mabilioni Dar

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kujihusisha na utapeli wa kuendesha mchezo wa upatu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema walinasa watu hao Septemba 29, mwaka huu saa 7 mchana.

Kazi hiyo ilifanikishwa na taarifa za msiri wao aliyewaambia kwamba maeneo ya Chanika kuna watu wanakusanya fedha kutoka kwa wananchi. Alisema watu hao walikuwa wakiwadanganya kuwa kuna fedha nyingi zimewekwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ambazo watagawiwa kama wanachama hai baada ya kutoa viingilio vya uanachama Sh 450,000 kila mmoja kitu ambacho si cha kweli.

Kwa mujibu wa Kamanda Mambosasa, msiri huyo alisema alipata taarifa kuhusu uwepo wa fedha BoT na kwamba Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Polycap Kardinali Pengo alitakiwa kusaini barua iliyoonesha imetoka Kampuni ya Funfumark Investment, Agosti 18, mwaka huu.

‘’Barua hiyo ilitakiwa kwenda kwa Gavana wa Benki Kuu ili fedha hizo zihamishwe kutoka Benki Kuu ya Tanzania kwenda Benki ya Mkombozi kiasi cha Sh Trilioni 250 ambapo wanachama hao wangegawiwa kama Amana na mali za “Tunu Discoveries Group,” alisema.

Alisema baada ya taarifa hizo ufuatiliaji ulianza ambapo askari walikwenda kwenye ofisi hizo na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne ambao ni wafanyakazi na viongozi wa kampuni hiyo.

Aliwataja watu hao kuwa ni Jackson Jeruman ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji, Abubakar Kaitaba Mkurugenzi Msaidizi, Israel Mwina Katibu pamoja na Mariam Bakari Mhasibu. Alisema katika upekuzi walipata mafaili 525 ya watu waliotoa fedha zao kiasi cha Sh 450,000 kila mmoja kwa ajili ya kufungulia akaunti na kwa ajili ya ofisi ya Funfmark.

Pia walipatikana na fedha taslimu Sh milioni 6,824,000 na dola 100 za Marekani zilizokuwa zimekusanywa kwa siku hiyo toka kwa wanachama. Alisema katika mahojiano ya awali watuhumiwa wameeleza “Tunu” zinazoongelewa ni kutokana na imani yao ya kidini na ndoto walizooteshwa na lengo la kukusanya fedha kutoka kwa wanachama hao walikuwa na nia ya kujenga makanisa na misikiti kwa ajili ya waumini wa madhehebu yote Tanzania.

Aliongeza kuwa watuhumiwa hao wameshindwa kuthibitisha Tunu wanazoongelea kuwekwa BoT au uhusiano wao na Kardinali Pengo kuwa ni msimamizi wa Tunu hiyo. “Kitu ambacho wamedanganya ni kwa kutumia majina ya Benki Kuu ya Tanzania na kutumia jina la Askofu Mkuu Kardinali Pengo wa Kanisa Katoliki kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha zaidi ya Sh milioni 122 na dola 2,200 za Marekani kutoka kwa wanachama waliojiunga kwenye kampuni yao ambapo hadi sasa kuna wanachama wapatao 875,” alisema Mambosasa.

Mambosasa alisema baada ya wanachama kuhojiwa walieleza kuwa, kuhusu kutoa fedha zao kwenye kampuni ya Funfmark waliamini kidini kuwa kweli baadaye wangeweza kupata fedha nyingi kutoka kwenye Amana za Tunu iliyoko BoT pia walikuwa na imani kwamba fedha zao walizotoa zinatumika katika kufungua akaunti ya Dola kwa ajili ya Kampuni, kwani fedha za Amana zilizopo Benki Kuu ni Dola na baadaye kila mwanachama angeingiziwa gawio kwenye akaunti yake binafsi.

Alisema upelelezi unaendelea kwa kupata maelezo ya wanachama hao waliotapeliwa na kupata vielelezo kutoka kwa Msajili wa Kampuni, BRELA, pamoja na Wizara ya Maliasili na Utali idara ya Utafiti wa mali kale.