Watanzania waliofungwa kwa mihadarati China wapungua

KUTOKANA na juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kupambana na biashara ya dawa za kulevya, tangu kuingia madarakani ni Watanzania wanne tu waliokamatwa na dawa hizo nchini China ambayo asilimia 90 ya Watanzania wamefungwa kwa kujihusisha na mihadarati.

Wakati katika magereza nchini humo kuna wafungwa 217, asilimia 90 ya wafungwa hao wamefungwa kwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Aidha, imefahamika kuwa hakuna Mtanzania aliyewahi kunyongwa nchini humo au kuhukumiwa kunyongwa, bali wengiwanahukumiwa vifungo vya maisha au vifungo vya miaka mitano hadi 25. Kupungua kwa Watanzania kukamatwa na kufungwa China, kumetokana na mikakati mbalimbali ya Serikali ya Awamu ya Tano na ile ya Awamu ya Nne kwani mpaka kufikia Septemba mwaka huu, ni Watanzania 217 ndiyo wamefungwa gerezani nchini China, lakini hakuna aliyehukumiwa kunyongwa.

Taarifa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini China zinaeleza kuwa wafungwa hao ni kutokana na makosa mbalimbali, lakini wengi wao wakikamatwa kwa kuhusiana biashara ya dawa za kulevya, kusafirisha kutoka Tanzania, kusafirisha ndani ya China kutoka mji wa Guangzhou kwenda Beijing na wengine kuuza ndani ya nchi hiyo.

Imeelezwa kuwa mwaka huu ni Watanzania wanne tu walikamatwa na dawa hizo wote katika mji wa Guangzhou ambao walikamatwa kuanzia Januari hadi Aprili kwa kuuza dawa ndani ya nchi hiyo, hivyo hakuna aliyekamatwa kutoka Tanzania hivyo kusaidia kudhibiti nchi kuonekana ni sehemu ya kusafirishia dawa. Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki alieleza kuwa idadi ya wafungwa Watanzania wanaohusika na biashara ya dawa za kulevya nchini humo, imepungua kwa kasi kutoka 34 mwaka 2013 hadi mwaka jana hakukuwa na Mtanzania aliyekamatwa kwa tuhuma hizo huku mwaka huu wakikamatwa wanne ndani ya China.

Balozi Kairuki alisema Watanzania waliofungwa nchini humo, wamekamatwa katika maeneo matatu ambayo yana sheria na utawala tofauti ambayo ni Jamhuri ya Watu wa China (PRC), Hongkong na Macao na takwimu zinaonesha wafungwa 264 waliwahi kufungwa kuanzia mwaka 2005 na wengi wao wakiwa ni dawa za kulevya.

Kati ya wafungwa hao, 110 walifungwa China PRC, 80 kifungo cha maisha na wanawake wakiwa 35 katika yao 89 wakiwa kwa kuingiza dawa za kulevya nchini humo na wengine makosa mbalimbali. Alieleza kuwa kati ya wafungwa hao, 95 wanaendelea na vifungo vyao kwa makosa mbalimbali huku 15 wakitoka nje kwa watatu kumaliza vifungo, mmoja kukosekana ushahidi, wanne walirudishwa Tanzania kwani walikuwa wamekaa muda mrefu bila kibali, wanne ambao walikuwa wanafunzi waliondolewa nchini kwa kufanya fujo na kudaiwa biashara ya dawa ya kulevya wakiwa vyuoni huku watatu wakitolewa baada ya kupata dhamana.

Alieleza kuwa huko Hongkong kwa kipindi hicho, walikamatwa Watanzania 139 na kati yao 135 kwa kuingiza dawa za kulevya, huku wanawake wakiwa 35 na wanne wakifungwa kwa wizi mpaka sasa wamebaki wafungwa 114 na waliotoka ni 20. Alisema Macao walikuwa 15 wote walikamatwa kwa kuingiza dawa za kulevya, wanawake wakiwa watatu na saba tu ndiyo wametoka na kubaki wanane.

Balozi Kairuki aliongeza kuwa hakuna Mtanzania aliyewahi kunyongwa nchini humo au kuhukumiwa kunyongwa, bali wengi wanahukumiwa vifungo vya maisha au vifungo vya miaka mitano hadi 25. Alisema hatua hiyo inatokana na kuwa hukumu ya kunyongwa kwa watuhumiwa wa dawa za kulevya ni kwa Jamhuri ya Watu wa China pekee, lakini kwa Hongkong na Macao hawana hukumu hiyo.

Alieleza bayana kuwa si jambo la kushangaza kwa Watanzania waliokamatwa na dawa hizo, kutonyongwa katika utawala huo wa China kwa kuwa wana sheria kuwa ikiwa mtuhumiwa atakaa miaka miwili baada ya kuhukumiwa kunyongwa na utekelezaji haujafanyika, kifungo hicho inakuwa cha maisha.

Alisema pia lakini nchini China, kuna Sheria ya ‘Parole’ ambayo wanamuangalia tabia ya mfungwa tangu akiingia jela kila mwaka na kupewa vigezo vinavyoangaliwa kisha kupewa alama na zikifika kiasi fulani anapunguziwa kifungo cha maisha na kuwa cha miaka kadhaa. Alisema sheria hiyo, pia inawahusu wale wa miaka kadhaa, hivyo si jambo la ajabu nchini humo mtu aliyefungwa maisha akawa huru.

“Wakiwa magerezani wafungwa nchini hapa wanalipwa kila mwezi pesa za China Yuan 200 hadi 300 (sawa na elfu 60,000 hadi 100,000 za Tanzania) kutokana na uzalishaji wanaofanya kama kushona nguo, viatu na kutengeneza vitu mbalimbali,” alieleza.

Pia wapo wengine wakipata nafasi ya kusoma katika viwango mbalimbali, na kuna Mtanzania amemaliza Shahada huko Hongkong na anaendelea kusoma Shahada ya Uzamili. Alieleza kuwa nchini humo raia wa kigeni, akikamatwa kwa makosa mbalimbali, lazima ubalozi upewe taarifa kwa maandishi na kuelezwa gereza atakaloenda na ikifika wakati wa hukumu wanaelezwa pia.

“Hata taarifa kwa ndugu ni lazima ubalozi kuhakikisha na kuitaarifu magereza ili aruhusiwe kuwasiliana na ndugu husika na hata kumuona mfungwa ni mpaka usajiliwe ili uweze kumuona hivyo tunashangaa na baadhi ya takwimu za wafungwa zinazotolewa ambazo siyo sahihi,” aliweka wazi Balozi Kairuki.