Polisi: Hatutaki malumbano na familia ya Lissu

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amesema jeshi hilo halitaki malumbano na familia ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na kwamba jeshi hilo linafanya kazi zake kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria kuwahudumia wananchi.

Aliyasema hayo alipozungumza na waandishi jijini Mbeya wakati akijibu swali kama ni kweli jeshi hilo limeshindwa kuwakamata watuhumiwa waliompiga risasi mbunge huyo na familia yake kudaiwa kutaka wachunguzi kutoka nje ya nchi wahusishwe. Sirro alisema hana majibu kuhusu swali hilo kwa sababu hataki malumbano.

“Jeshi lipo kwa ajili ya Watanzania wote, nchi ipo shwari, kama kuna mtu anafikiria hivyo na mimi ndiyo Mkuu wa Jeshi la Polisi nawajibika kwa usalama wa raia na mali zao,” alieleza IGP Sirro.

Akizungumzia hali ya ulinzi na usalama, IGP Sirro alisema kuna changamoto ya mauaji yanayotokana na imani za kishirikina pamoja na mauaji ya watu yanayofanywa na watu wanaojiita wenye hasira kali. “Mpango wetu ni kutoa elimu kwa wananchi waachane na imani za kishirikina na mauaji ya watu wenye hasira kali kwa kuwa sheria zipo,” alisema IGP Sirro na kuongeza kuwa watawashirikisha wanasiasa na viongozi wa dini katika kutoa elimu kwa wananchi.