Magufuli, Kenyatta wazika vikwazo vya biashara

WIZARA za Mambo ya Nje za Kenya na Tanzania zimetekeleza maagizo wa marais wa nchi hizo, Dk John Magufuli wa Tanzania na Uhuru Kenyatta wa Kenya, kwa kuagiza unga wa ngano kutoka Tanzania, uingie Kenya bila vikwazo na usitozwe ushuru.

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji anayeshughulikia Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda alisema jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kuwa, mawaziri wa wizara hizo pia wameagiza gesi ya Tanzania iruhusiwe kuingia Kenya bila vikwazo. Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, viongozi hao pia wameagiza maziwa, bidhaa za maziwa, na sigara kutoka Kenya ziruhusiwe kuingia nchini bila vikwazo na jitihada zifanyike kuondoa vikwazo vingine vyote vya kibiashara baina ya nchi hizo.

Rais Magufuli na Kenyatta waliagiza hatua zichukuliwe kumaliza mvutano na kuondoa vikwazo vingine vya biashara baina ya nchi hizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja la Kenya na Tanzania kwa vyombo vya habari, iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya hivi karibuni, marais wa nchi hizo wamekubaliana kwamba, Kenya iondoe vikwazo kwenye kuingiza unga wa ngano na gesi kutoka Tanzania.

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa Rais Magufuli na Kenyatta, wamekubaliana kwamba Tanzania iondoe vikwazo mara moja katika kuingiza maziwa, bidhaa za maziwa na sigara kutoka Kenya. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kenya na Tanzania zimekubaliana kuondoa vikwazo vingine vyovyote vinavyoathiri upatikanaji wa bidhaa na huduma baina ya nchi hizo.

Wakuu hao waliwaagiza mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo, kutoa taarifa ya pamoja kutangaza uamuzi wao (kwa wakuu wa nchi) Julai 14 mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Augustine Mahiga na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohammed walikutana Dar es Salaam kuzungumzia utekelezaji wa maagizo hayo. Julai 23 mwaka huu, Waziri Mahiga na Waziri Amina walikutana Nairobi, Kenya kuzungumzia utekelezaji huo. Profesa Mkenda alisema mwanzoni mwa Septemba mwaka huu Kenya na Tanzania zilifanya mazungumzo jijini Dar es Salaam kuhusu masuala ya biashara hususan changamoto za kibiashara kati ya nchi hizo zilioongezeka mwanzoni mwa mwaka huu.

“Kwa kweli tulifika mahala ambapo si pazuri na ilikuwa lazima hatua zichukuliwe kumaliza suala hili. Hiyo ndiyo hali tuliyokuwa nayo mwezi wa Juni. Mahusiano ya kibiashara baina yetu na Kenya yalidorora na yalikuwa yanaelekea kudorora zaidi, kwa sababu tusingekubali kabisa sisi kuwa ni gulio la Kenya kuuzia bidhaa zake wakati sisi tumewekewa vizingiti kuuza bidhaa zetu Kenya,” alisema Profesa Mkenda. Alisema, mazungumzo yalikuwa marefu na magumu, lakini yaliendeshwa kwa urafiki uliozingatia mahusiano ya nchi hizo.

“Siku ya mwisho ya mazungumzo haya tulianza asubuhi mpaka jioni na kuendelea usiku mzima mpaka alfajiri siku iliyofuata. Tulipata mafanikio mazuri. Kenya walileta mezani masuala kumi na sita, sisi tuliweka mezani masuala kumi na tano. Baadhi ya masuala haya yalihitaji tu ufafanuzi, na tulifanikiwa kubadilishana mawazo na kukubaliana kuhusu ufafanuzi,” alisema. Profesa Mkenda ndiye aliongoza ujumbe wa Tanzania uliojumuisha maofisa waandamizi wa Serikali kutoka wizara mbalimbali, wafanyabiashara na wakulima wa ngano.

Alisema, Tanzania ilitekeleza maagizo ya mawaziri wa mambo ya nje ikiwa ni pamoja na kuruhusu maziwa na bidhaa za maziwa kutoka Kenya kuingia Tanzania bila vikwazo na bila ushuru. “Kuhusu sigara, ni vizuri nieleze kwamba hatujazuia na hatukuwahi kuzuia sigara kutoka Kenya kuingia Tanzania. Kulikuwa hakuna kabisa kizuizi cha kuingiza sigara kutoka Kenya. Hata hivyo sheria yetu inatoa unafuu wa kodi kwa sigara ambazo zinazalishwa nchini kwa kutumia walau asilimia sabini na tano ya tumbaku inayolimwa hapa nchini,” alisema.

Aliongeza kuwa, kuna sigara zinazozalishwa nchini zisizotumia kiwango hicho cha tumbaku ya nchini hivyo hazipati unafuu huo wa kodi. “Kadhalika sigara kutoka nje ya nchi hazipati unafuu huu wa kodi. Wenzetu wa Kenya wanalalamikia jambo hili, kwamba linafanya sigara zao zisiweze kushindana ndani ya soko la Tanzania, na kwamba ni kinyume cha taratibu za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki,” alisema. Alisema, hoja ya Kenya ina mantiki kiasi, lakini jambo hilo haliibagui Kenya tu, ni kwa sigara zote kutoka nje, lakini suala hilo ni la kisheria hivyo haliwezi kubadilishwa hadi Bunge liibadili sheria husika.

“Hata Kenya nao wanao utaratibu huu kwa aina fulani ya bia. Kuna aina ya bia huko Kenya ambayo inapata unafuu wa kodi endapo tu itatumia nafaka iliyozalishwa Kenya, jambo ambalo pia linasababisha bia kutoka Tanzania zisiweze kuwa shindani kwenye soko la Kenya. Kwa vyovyote vile, suala la sigara lisingeweza kutatuliwa kirahisi,” alisema. Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, masuala ya unga wa ngano, gesi ya kupikia, maziwa na bidhaa za maziwa yalikuwa ni ya dharura, na ndiyo yaliyosababisha uhusiano wa kibiashara kati ya Kenya na Tanzania kudorora sana Juni mwaka huu.

Kiongozi huyo alisema, bado kuna changamoto za kibiashara baina ya Kenya na Tanzania na wamekubaliana wakutane Novemba kujadili changamoto zilizobaki. Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, mwishoni mwa Januari mwaka huu Kenya iliamua kutoza ushuru wa forodha kwa unga wa ngano unaoingia Kenya kutoka Tanzania kinyume na utaratibu wa forodha wa EAC.

“Unga wa ngano kutoka Tanzania ulipaswa kuingia Kenya bila kutozwa ushuru. Mwezi wa Tano mwaka huu Kenya iliamua kupiga marufuku uingizwaji wa gesi ya kupikia kutokea Tanzania. Marufuku hii ilikuwa haina sababu zozote za msingi,” alisema. Alisema mwishoni Mei mwaka huu mambo hayo yalizungumzwa kwa kirefu kwenye kikao cha mawaziri wa biashara wa EAC jijini Arusha na kwamba, viongozi hao walitoa uamuzi wa pamoja.

“Kwanza, iliamuliwa kwamba Kenya iache mara moja kuzuia gesi ya kupikia kuingia Kenya kutokea Tanzania. Pili, iliamuliwa kwamba utaratibu wa kuruhusu unga wa ngano kutoka Tanzania kuingia Kenya uanze pale Tanzania itakapoanza kutumia utaratibu wa duty remission katika uingizaji wa ngano kutoka nje ya Jumuiya. Jambo hili lilitakiwa liwe limekamilika tarehe mosi mwezi Julai” alisema. Alisema, mawaziri hao pia waliamua kuwa, Tanzania na Kenya zizungumze kutatua changamoto zote za biashara kati ya nchi hizo.

“Haya ndiyo yaliyokuwa maamuzi ya kikao cha mawaziri wa biashara wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, maamuzi ambayo yalikubaliwa na nchi zote, ikiwa ni pamoja na nchi yetu na Kenya. Hata hivyo baada ya maamuzi haya Kenya iliendelea kuzuia gesi ya kupikia kutoka Tanzania kuingia Kenya, na wenzetu hawakutupa sababu za msingi za kukiuka maamuzi ya Arusha,” alisema.

Profesa Mkenda alisema, Tanzania iliamua kutofanya mazungumzo ya kibiashara na Kenya hadi nchi hiyo itekeleze makubaliano ya Arusha. “Tulifuta mwaliko tuliokuwa tumetuma Kenya wa kuja kufanya mazungumzo jijini Dar es Salaam na kuweka bayana kwamba hatutafanya mazungumzo katu kama maamuzi ya mazungumzo ya awali hayajatekelewa… Kenya ilianza kupata changamoto ya kuingiza baadhi ya bidhaa zake nchini mwetu, hasa maziwa na bidhaa za maziwa,” alisema.

Alitaja malalamiko megine ya Kenya kuwa ni Tanzania ilikuwa inakisia kiwango cha juu thamani ya juisi kutoka Kenya, lakini baada ya maelezo na ufafanuzi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA) walikubali kwamba makisio yaliyokuwa yamefanywa na Tanzania yalikuwa sahihi hivyo, suala hilo liliisha. “Kuna mambo mengine tumekubaliana kwamba yatafanyiwa kazi kwa haraka.

Kwa mfano, Tanzania tuna sababu ya kuamini saruji kutoka Kenya haikidhi viwango vya uasilia- yaani rule of origin, kwa hiyo hatujakubali saruji hii inufaike na unafuu wa forodha wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Upo utaratibu wa kutatua utata wa masuala ya uasilia na tumekubaliana utaratibu huu ufuatwe mara moja,” alisema. Alisema Kenya ni wadau muhimu kibiashara, hivyo serikali za nchi hizo zimekusudia kuondoa