Mfumuko wa bei Tanzania sasa 5.3%

MFUMUKO wa bei wa Taifa umeongezeka hadi kufi kia asilimia 5.3 kwa Mwezi Septemba 2017 kutoka asilimia 5.0 Mwezi Agosti mwaka huu.

Ongezeko hilo limetokana na kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Septemba, 2017 ikilinganishwa na mwaka ulioishia Agosti, 2017. Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraim Kwesigabo alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 0.02 kwa Mwezi uliopita ikilinganishwa na kupungua kwa asilimia 0.4 mwezi Agosti mwaka huu.

Imeelezwa kuwa ongezeko la asilimia 0.02 la mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi limetokana na kuongezeka kwa fahirisi za bei (namna bei zinavyopanda) kutoka uniti 108.46 mwezi Agosti hadi kufikia uniti 108.48 mwezi uliopita, ambapo tofauti ya uniti hizo ndiyo imeleta ongezeko la asilimia 0.02. Kwa mujibu wa Kwesigabo, kuongezeka kwa fahirisi za bei kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.

Alizitaja baadhi ya bidhaa hizo kuwa ni dagaa kwa asilimia 7.6, matunda makavu kama nazi kwa asilimia 3.1, viazi vitamu kwa asilimia 3.0, mchele kwa asilimia 1.5 na ndizi za kupika kwa asilimia 1.5. Kwa baadhi ya bidhaa zisizo za chakula alizozitaja kuchangia kuongezeka kwa fahirisi ni pamoja na mkaa kwa asilimia 4.0, dizeli kwa asilimia 2.4 na petroli kwa asilimia 0.6.

Naye Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Stephen Kirama alisema kuwa mfumuko wa bei unapoongezeka maana yake uwezo wa watu kununua bidhaa unakuwa umeshuka na hivyo kuathiri ubora wa maisha wanayoishi. Alisema mfumuko wa bei unaweza kusababishwa na mambo mengi lakini mojawapo ni kupungua kwa uwezo wa kuuza nje bidhaa.

Kwa kulinganisha hali ya mfumuko wa bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki hasa Tanzania, Kenya na Uganda, Kwesigabo alisema kuwa Tanzania na Uganda kwa mwezi uliopita mfumuko wa bei uliongezeka kwa asilimia 5.3 ikilinganishwa na Kenya ambako mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 7.06 mwezi uliopita ikilinganishwa na asilimia 8.04 mwezi Agosti. Kuhusu thamani ya Shilingi ya Tanzania, Meneja wa Takwimu za Ajira na Bei kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ruth Minja alisema kuwa uwezo wa Shilingi ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma hupungua ikiwa Fahirisi za bei za taifa huongezeka.