DPP aagiza Raila Odinga, Musyoka wachunguzwe

MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP) wa Kenya, Keriako Tobiko amewapa Polisi siku 21 wawachunguze viongozi wa upinzani, Raila Odinga na Kalonzo Musyoka kutokana na kauli zao kwamba, hakutakuwa na uchaguzi wa Rais Oktoba 26.

Alitoa agizo hilo baada ya Wakili Harrison Kinyanjui kulalamika kwa niaba ya Samuel Waweru Gikuru na kutaka wanasiasa hao wachunguzwe. Tobiko amemwandikia Mkurugenzi wa Upelelezi Makosa ya Jinai (DCI), Ndegwa Muhoro akimwelekeza afanye uchunguzi kwa kina na uliokamilika kuhusu tuhuma hizo na kuripoti kwake ndani ya siku 21.

“Uchunguzi ukamilike na mafaili ya matokeo ya uchunguzi yawasilishwe kwenye hii ofisi ndani ya siku 21 ili yapitiwe na maelekezo sahihi,” aliagiza DPP kwenye barua hiyo ya Oktoba 2, mwaka huu. Kinyanjui alihitaji Odinga na Musyoka wachunguzwe, wakamatwe na washitakiwe kwa kutoa kutoa kauli zilizojirudia kwamba, hakutakuwa na uchaguzi wa Rais Oktoba 26 mwaka huu.

Alisema, kauli hizo zinakiuka kifungu cha 13 cha Sheria ya Makosa ya Uchaguzi. Kwa mujibu wa Wakili huyo, kauli za wanasiasa hao zinakiuka pia kifungu cha 131 na 132 cha Kanuni za Adhabu kwa kuwaghasi na kuwatisha maofisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Kwa mujibu wa DPP, imeundwa timu ya waendesha mashitaka ili itoe msaada wa kiufundi na maelekezo kwa timu ya wachunguzi.