Viziwi: Tunaathirika kwa noti bandia

Tatizo la kutosikia na kukosa elimu ya utambuzi wa noti bandia limedaiwa kuwa chanzo cha watu wenye ulemavu wa kusikia (viziwi) kupoteza mitaji, biashara na kuathirika kiakili.

Mwenyekiti wa Kituo cha Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi Tanzania (Kisuvita), Habibu Mrope aliyasema hayo jana jijini hapa kupitia mkalimani wakati wa ufunguzi wa elimu kwa umma kwa viziwi juu ya utambuzi wa noti bandia iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT). Mrope alisema viziwi ni waathirika wakubwa wa noti bandia kutokana na kutozitambua noti hizo.

“Waovu wamekuwa wakiwalenga viziwi kwa kuwa wanafahamu hawana elimu ya kuzitambua noti bandia na wamekuwa wakibambikiwa wakati wa kununua au kuuza bidhaa,” alisema. Meneja Msaidizi wa Idara ya Uhusiano wa BOT, Vicky Msina alisema elimu wanayoitoa imelenga kuwawezesha viziwi kutambua alama za usalama zilizopo katika noti ili kuzitofautisha na noti bandia wanapokuwa katika shughuli zao. Alisema, “Mtu akikutwa na noti bandia ni kosa la jinai, hivyo tunawapa mafunzo ili wasikumbwe na tatizo hilo.”