Wabunge, waziri mbaroni kwa kukacha bunge

WABUNGE wanne na waziri mmoja katika Jimbo la Gok, Sudan Kusini, wameripotiwa kuwa walishikiliwa kwa saa kadhaa, wakituhumiwa kukosekana katika kikao maalumu cha Bunge hivi karibuni.

Kwa mujibu wa John Marik Makur ambaye ni mbunge, wabunge hao walishikiliwa na vyombo vya usalama. Mbunge huyo alisikika akiyasema hayo kupitia kituo cha redio cha Eye. “Walishikiliwa.

Baadhi walikuwa na shughuli binafsi, wengine walikwenda hospitali, lakini kimsingi hawakuwa na taarifa za kikao hicho maalumu,” alikaririwa akisema. Walioshikiliwa wametajwa kuwa ni Waziri wa Miundombinu katika Jimbo hilo, Ayen Maan Ador, Mnadhimu Mkuu katika bunge, Santino Manyiel Mading na wabunge Simon Mayar Marial, Malek Machot Padai na Ater Machar.

Makur alidai kuwa, wabunge hao hawakuwa na taarifa za kikao na walishikiliwa wakati wakirejea makwao, hivyo kuibua mvutano na gavana wa jimbo. Spika wa Bunge, Umjima Phili alikiri kutiwa mbaroni kwa wanasiasa hao, lakini akasema walichukuliwa hatua hiyo kutokana na kufanya kikao kisicho rasmi nje ya bunge.

Jimbo la Gok ni moja ya maeneo ya Sudan Kusini yenye mapigano ya mara kwa mara. Sudan Kusini imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2013, miaka miwili baada ya Uhuru wake. Mpasuko huo unatokana na kutopikika chungu kimoja baina ya Rais Salva Kiir na aliyekuwa Makamu wake, Riek Machar anayeendesha mapigano akiwa msituni.