Uhaba wa madawati wadhibitiwa kwa 95%

WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako (pichani) amesema mpaka sasa asilimia 95 ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini, wanakaa kwenye madawati tofauti na ilivyokuwa miaka ya hapo nyuma.

Pia amesema matunda hayo yote yanatokana na serikali ya Rais John Magufuli yenye dhamira ya dhati katika kuboresha elimu nchini, ambapo imefanya mambo ambayo hayakuwa yamefanywa tangu nchi ipate uhuru katika sekta hiyo ndani ya miaka miwili tu.

Profesa Ndalichako alisema hayo jana katika mahojiano maalumu na Kituo cha redio cha TBC Taifa, ambapo alisema jambo ambalo amelifanya Rais Magufuli lingeweza kufanyika miaka mingi, kwani halikuhitaji fedha bali maelekezo.

“Rais Magufuli wala hakuhitaji fedha katika hili, ni maelekezo tu kwa hiyo ni ule utayari tu na katika hili tunampongeza sana Rais wetu,” alisema Profesa Ndalichako huku akisema kuwa changamoto ya madawati ni ndogo sana na kwa maeneo madogo.

Lakini, pia waziri huyo alisema katika Sera ya Elimu Bure, ambayo serikali inaitekeleza sasa, imeongeza idadi kubwa ya wanafunzi na kwamba serikali inaendelea kuhakikisha walimu na miundombinu inatosheleza mahitaji.

“Lakini kitendo cha wanafunzi kuwa wengi inathibitisha kwamba watu walikuwa hawaendi shule kwa sababu hawana ada, kwa sasa serikali imefanya jitihada kubwa kuhakikisha wanafunzi wanabaki shuleni,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema serikali mpaka sasa imejenga madarasa 1,400 kwa mwaka wa fedha uliopita. Mwaka huu imepanga kujenga madarasa zaidi ya 2,000. Pia imepanga kujenga matundu ya vyoo 3,394 na mabweni 261.

Elimu ya msingi na sekondari Katika elimu ya msingi, Profesa Ndalichako alisema dhana elimu ya msingi ni miaka saba na hiyo haijabadilika, ingawa kuna miaka ambayo mwanafunzi anatakiwa kupita katika elimu ya awali ili kuandaliwa.

Kuhusu elimu ya sekondari, alisema bado utaratibu wa serikali ni ule ule wa kwamba mtihani wa kidato cha pili lazima mwanafunzi afanye na asipofaulu ataruhusiwa kurudia mara mbili baada ya hapo kutakiwa kwenda shule za ufundi.

Aidha, alisema kwa sasa Baraza la Mitihani linapanga ufaulu katika mfumo wa daraja, ambapo awali ilikuwa ikiangaliwa wastani na kwamba mtihani huo umewekwa ili wanafunzi wasome kwa bidii. Profesa Ndalichako alisema elimu kwa sasa inaridhisha, kwani lengo la Rais John Magufuli ni kuhakikisha elimu inaimarishwa na kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye, ambapo kuendana na dhana ya uchumi wa viwanda.

“Kazi kubwa imefanyika kutoa mafunzo kwa walimu, kuboresha miundombinu kutoa zana za ufundishaji, kuondoa vikwazo kwa watu wenye mahitaji maalumu,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema kwa kuzingatia sera ya uchumi wa viwanda, serikali imehakikisha shule zote saba za ufundi zilizopo nchini, zinarudi katika hali nzuri, kwa kuzifanyia ukarabati na kuboresha maabara na karakana.

Alisema mkakati wa serikali ni kwamba shule hizo, ambazo zilikuwa zikichukua pia wanafunzi wa masomo mengine, zirudi kufundisha ufundi pekee na kuwatafutia nafasi nyingine wanafunzi wa taaluma nyingine, waliokuwa katika shule hizo.

“Kwa mfano shule ya Ifunda ambako ilikuwa ikichukua wanafunzi wengine pia wa masomo ya sanaa, tutajenga shule nyingine tuwahamishie ili mabadiliko yetu yasije kuleta athari tukawa tumepunguza nafasi za masomo kwa wanafunzi wengine, shule itakamilika mwaka huu wa fedha,” alisema Profesa Ndalichako.

Akizungumzia ufaulu mdogo wa wanafunzi katika masomo ya sayansi, alisema serikali inaendelea kuhamasisha na kuongeza nafasi kwa wanafunzi wanaosoma masomo hayo, ingawa changamoto kubwa iko katika somo la Hisabati.

“Ukiangalia hata katika mtihani uliopita ufaulu ni asilimia 16 katika somo la Hisabati na hiyo ni katika alama A hadi D, lakini katika masomo ya Kemia, Fizikia na Baolojia ufaulu na idadi ya wanafunzi wanaosoma inaridhisha, mwitikio upo,” alisema.

Aidha, alisema pia serikali imepandisha daraja shule 28 kwa kuongeza kidato cha tano na sita na kuboresha miundombinu. Alisema changamoto ilikuwa ni wanafunzi kufundishwa kwa nadharia bila vitendo, ambapo serikali imenunua vifaa vya maabara na kusambazwa katika shule 1,696 nchini. Lengo la hatua hiyo ni katika kuimarisha masomo ya sayansi.

Masomo ya sayansi na hisabati Katika vyuo vya ualimu, alisema serikali imeboresha vyuo vya ualimu 10 kwa ajili ya masomo sayansi na hisabati, kwa kununua vifaa na pia kuboresha mbinu za kufundishia na kupitia upya mitaala.

Profesa Ndalichako alitoa mwito kwa walimu kutumia mbinu bora za kufundishia kuwafanya wanafunzi kupenda masomo ya sayansi na hasa hisabati. “Wanafunzi wawe tayari kujifunza, mtu anaogopa kabla hata hajajaribu, hajaweka jitihada kwa sababu hakuna kitu kizuri kinakuja bila kugharamia kwahiyo mwanafunzi lazima ajibidishe na walimu wasikate tama, waendelee kuwahamasisha,” alisema.

Alisema wanafunzi ambao wanasoma masomo ya sayansi ni rahisi kuhamia kwenye masomo mengine na pia wanakuwa ni rahisi kupata chaguo nyingi vyuoni, kama walifanya vizuri katika masomo ya sayasi na hisabati.

Profesa Ndalichako aliwaasa pia walimu kutoa mazoezi ya kutosha kwa wanafunzi ili waweze kuzoea kanuni na namna ya kuzifanya. Adhabu kwa wanafunzi Alisema kuna Waraka wa Elimu wa mwaka 2002, ambao unazungumzia utoaji adhabu ya viboko shuleni, ambao unaonesha makosa ambayo yanafaa viboko na pia unafafanua kuwa mkuu wa shule, ndiye anayetakiwa kutoa adhabu hiyo au akachagua mwalimu.

“Adhabu inatolewa panapokuwa na kosa, lakini mimi ningependa kwamba kuwe na utii wa sheria bila shuruti, walimu na wanafunzi wawe marafiki waweze kujikita katika kusoma kuliko kuwa mahakama kwa kesi na adhabu, walimu nawasisitiza wazingatie waraka unaoelekeza kutoa adhabu,” alisema.

Vyuo vikuu Profesa Ndalichako alisema serikali inatarajia kutoa majina ya wanavyuo ambao ni wanufaika wa mikopo, kabla ya vyuo kufunguliwa na watapata fedha hizo wakifika tu kwenye vyuo.

“Ili mwanafunzi kabla hajasafiri, ajue kabisa amepata mkopo au la, na katika hili namshukuru sana Rais, serikali imeshatenga fedha hizo na tumejipanga vizuri hakutakuwa na changamoto za wanafunzi kufika na kukaa wiki mbili bila kupata fedha,” alisema.

Alisema wale ambao watakuwa hawakupata mkopo, ina maana hawajakidhi vigezo ambavyo ni pamoja na uhitaji, ambao hawajapata ni pamoja na wale ambao wanatoka katika familia zenye uwezo, wengine watoto wa viongozi,” alisema.

Vyuo vinatarajiwa kufunguliwa mwezi huu mwishoni. Alisema mwaka huu wanafunzi walikuwa wanaomba moja kwa moja kwenye vyuo ambavyo wanavitaka. Alisema tayari vyuo hivyo vimeshatoa majina, ingawa imejitokeza changamoto ya baadhi ya wanafunzi kukosa vyuo.

“Kuna wanafunzi pamoja na kwamba amepata ‘divisheni one’ lakini wamekosa vyuo, nitumie fursa hii kuwaambia kujiunga na vyuo ni ushindani, changamoto wanaomba kozi yoyote,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema changamoto nyingine ni wanafunzi wengi kuomba kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) huku kozi wanazoomba zina ukomo wa wanafunzi wanaochukua kwa mwaka, hivyo kufanya wengi kukosa kutokana na wingi wa maombi.

Alitoa angalizo kwa wanafunzi kuangalia kozi wanazoomba na idadi ya wanafunzi ambao wanachukuliwa kwa mwaka. Jana ilikuwa ukomo wa kutuma maombi katika vyuo kwa muda wa nyongeza. Awali ilikuwa Agosti 30 mwaka huu.

“Niombe sana vijana watulie katika kusoma maelekezo, tunaweka matangazo katika mitandao, mitandao tumieni katika kupata habari zinazowasaidia… ambao hawakupata vyuo kwa kutozingatia mahitaji mahsusi au kuchagua kozi zenye ushindani mkubwa watulie,” alisema.

Waziri huyo aliwaasa pia wanafunzi watakaopata mkopo, waitumie vizuri ambazo wanahitaji na nyingine kuziacha, kwani huo ni mkopo. Alitaka wasitumie fedha hizo kwenye anasa na pia waache kuishi maisha ya kufuata mkumbo.