Kairuki aapa kudhibiti utoroshaji madini

SIKU moja baada ya kuapishwa, Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ameweka bayana kuwa kipaumbele chake kikuu katika wizara hiyo ni kudhibiti utoroshaji wa madini nchini.

Kairuki alisema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na watumishi wa Wizara ya Madini pamoja na taasisi zake, waliopo Dar es Salaam na Makao Makuu ya Wizara Dodoma. Pia baadhi ya taasisi zilizoshiriki katika kikao hicho ni Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Chuo cha Madini Dodoma (MRI) na Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini na Mpango wa Kuongeza Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji (TEITI).

Waziri huyo alisema kuwa lengo la kikao hicho lilikuwa ni kufahamiana na kupanga mikakati ya kushirikiana ili kuhakikisha kuwa sekta ya madini inakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Lakini, pia waziri huyo ambaye alikuwa akihudumu kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, pia alizungumza kuhusu maslahi kwa wafanyakazi huku akiwataka watumishi kufanya kazi kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu.

Alisema kuwa, “Sekta ya Madini inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa wa ukuaji wa uchumi wa nchi na hivyo ninawataka wataalamu wa madini kubuni mbinu za ukusanyaji wa maduhuli pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye uchimbaji madini.”

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo aliwakumbusha watumishi kuzingatia dira na dhima ya wizara, ikiwemo kufanya kazi kwa tija ili hatimaye sekta ya madini iweze kuchangia katika uchumi wa nchi kwa kuwa mchango wa sekta husika bado ni kidogo