Wazee watakiwa kukomesha ukatili

WAZEE wa mila wilayani hapa wametakiwa kuamua kwa nguvu moja kushiriki katika kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya mtoto wa kike, ikiwemo mimba za utotoni na ndoa ili kundi hilo liweze kukua na kufikia ndoto zao pamoja na kuchangia katika uchumi wa viwanda.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga alisema hayo jana wilayani hapa katika majadiliano ya Jukwaa la Mtoto, ambalo limeandaliwa na wadau mbalimbali wakiwemo Shirika la Plan International, ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani inayoadhimishwa leo.

Kitaifa siku hiyo inaadhimishwa katika wilaya ya Tarime mkoani Mara na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu atakuwa mgeni rasmi.

Akizungumza, Luoga alisema wazee wa mila katika wilaya hiyo ni watu muhimu sana katika kutokomeza vitendo vya ukatili kwa mtoto wa kike ikiwa in pamoja na kuzuia mimba za utotoni na ndoa ambazo huwazuia kufikia ndoto zao. “Wazee wa mila kama mlivyoweza kuhamasishana na kutumia madaraka yenu na kuzuia migogoro na mapigano ya koo mbali mbali yaliyofanyika wakati huo, vilevile mkiamua hata suala la mimba za utotoni na ndoa kwa Watoto wa kike mnaweza pia kudhibiti,” alisema Luoga.

Alisema wakati wa kuadhimisha siku ya mtoto wa kike, tatizo la mimba za utotoni na ndoa limekuwa likishamiri sana maeneo mbalimbali nchini na kwa takwimu za mwaka huu kwa wilaya ya Tarime watoto 21 wameacha shule huku ndoa zikiwa ni mbili.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mtoto wa Wizara ya Afya, Margaret Mussai alisema katika kuadhimisha siku ya mtoto wa kike, serikali ina mpango kazi ambao unatekelezwa utakaohakikisha unapunguza mimba za utotoni kutpka asilimia 27 iliyopo sasa na kufikia asilimia tano katika mwako 2021.

Meneja wa Plan International Tawi la Mwanza, Baraka Mgohamwende alisema shirika hilo linatoa elimu mbalimbali kwa jamii ya Tarime, mafunzo, majadiliano mashuleni ili kuamsha watu kupinga ndoa za utotoni na hata mimba za umri mdogo