Simu, kompyuta vyatajwa chanzo matatizo ya macho

MATUMIZI ya simu za mkononi na kompyuta kwa muda mrefu, yametajwa kuwa ni miongoni mwa sababu zinazosababisha ongezeko la magonjwa ya macho nchini kutokana na mionzi ya mwanga mkali iliyopo kwenye vifaa hivyo.

Hayo yamesemwa na Msimamizi wa Hospitali ya matibabu ya macho ya ‘International Eye Hospital’ ya Dar es Salaam, Adam Mwatima. Mwatima amesema chanzo kingine ni ongezeko la umri, hasa kwa watu wenye miaka zaidi ya 40 ambao wanakuwa kwenye hatari zaidi ya kupata tatizo la macho, hivyo hutakiwa kuonana na daktari mara kwa mara.

Alisema hayo Dar es Salaam juzi, wakati akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Macho duniani Oktoba 12 ya kila mwaka. Alisema katika maadhimisho ya mwaka huu, hospitali hiyo itatoa punguzo la gharama za utoaji wa huduma ya upimaji na matibabu kwa watu wote kwa asilimia 25 ya gharama husika.

“Kuna changamoto kubwa ya magonjwa ya macho katika maeneo mengi nchini kutokana na ongezeko la umri, matumizi makubwa ya simu za mkononi pamoja na kompyuta kutokana na mionzi ya mwanga uliopo kwenye vifaa hivyo,” alisema.

Alieleza kuwa lengo la hospitali hiyo ni kuisadia Serikali kutoa huduma bora za matibabu ya macho kwa wananchi wa kada zote kwa gharama nafuu, kwa kutumia wataalamu waliobobea katika huduma ya matibabu ya macho duniani kutoka Uingereza na Tanzania.

Hatua hiyo itaipunguzia gharama serikali ya kusafirisha wagonjwa wa macho kwenda nje ya nchi kwa matibabu, ikiwamo upasuaji kwani huduma hiyo kwa sasa inapatikana nchini kwa gharama nafuu.

Mkurugenzi wa Masoko wa hospitali hiyo, Ilakoze Bidyangize alisema hospitali hiyo pia inapokea watu wanaotumia huduma za bima za afya mbalimbali, ikiwamo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambapo mgonjwa anaweza kupimwa na kupata matibabu ikiwamo upasuaji.