Shule kuweka madawati ya ulinzi wa watoto

SERIKALI imeziagiza shule zote nchini za sekondari na msingi, kuanzisha madawati ya ulinzi na usalama wa mtoto katika shule zao ndani ya miezi sita kuanzia sasa ili mtoto akipata shida ajue atakakokwenda kutoa taarifa.

Aidha imezindua kampeni kwa mikoa 10 ya Tanzania Bara, ambayo itahakikisha inatokomeza mimba za utotoni, ikihamasisha Watoto wa kike kujilinda, kujithamini na kujipenda ili kufikia matarajio yao. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hayo wilayani hapa katika kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani.

Katika maadhimisho hayo, wadau mbali mbali wameshiriki katika maandalizi ya siku hiyo ikiwemo Plan International na wengine ambapo kauli mbiu ya siku ya mtoto wa kike ni Tokomeza Mimba za Utotoni kufikia uchumi wa Viwanda.

Ummy aliagiza kuwa ni lazima shule zote za msingi kuanzisha madawati hayo ya ulinzi na usalama wa mtoto ili mtoto ajue akipata tatizo la ukatili ikiwemo, ubakaji, ukeketaji ajue atakimbilia kwa mwalimu yupi au ofisi gani ili atoe taarifa na kusaidiwa.

Alisema mbali ya kuanzishwa kwa madawati hayo, pia walimu wakuu wachague mwalimu mmoja amani wawili ambao watahakikisha kuhusika katika dawati hilo. Kuhusu kampeni alisema serikali imezindua kwa mikoa 10 nchini ili kutokomeza mimba za utotoni ambayo itawezesha watoto wa kike kujitambua thamani waliyo nayo.

Alisema kwa mujibu wa Takwimu za Benki ya Dunia zinaeleza kuwa endapo wasichana wakiwezeshwa wanaweza kuchangia katika uchumi kwa asilimia 15 wakati kwa upande wa wanaume ni kwa asilimia 11.

Alisema kampeni ni endelevu ikigusa mikoa hiyo kwa Tanzania bara ili mtoto wa kike asome kwa bidii,huku akisisitiza kuwa serikali ina mpango pi waa kufanya utafiti ili kuwatambua mafataki wanaoharibu malengo ya mtoto wa kike na kuwachukulia hatua.

Aidha imewakumbusha wajibu wa walimu wakuu katika shule za sekondari na msingi nchini kutekeleza jukumu la kupeleka taarifa za wanafunzi wanaopata mimba kila baada ya miezi mitatu kwa Kamishna wa Elimu.

Ummy alisema mimba za utotoni zina athari kubwa, ambapo asilimia 15 ya vifo vya uzazi vinatokana na watoto kupata ujauzito kwa umri mdogo ambapo vifo hutokea kwa wenye umri kati ya miaka 15 hadi 18.

Awali akizungumza, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Watoto Duniani (UNICEF), Maniza Zaman alisema bado tuna kazi ya kufanya katika kuhakikisha mtoto wa kike aliye katika umri wa balehe anavuka kipindi hicho kwa usalama ili kufikia utu uzima.

Alisema ipo haja ya kulelewa kwa watoto wa kike na kiume tofauti na ilivyozoeleka awali, wakielezwa mazuri ambayo wazazi wao wameyapitia lakini yakiachwa yale yanayochangia ubaguzi na kuleta madhara kwa watoto wa kike.

Maghariba 63 waacha kazi, wasichana 2,166 waelimika Tarime Katika kilele cha siku ya mtoto wa kike duniani, jumla ya ghariba 63 wameelezwa kuacha kufanya kazi ya ukeketaji kwa watoto na kuanza mafunzo ya ujasiriamali utakaowasaidia kujiongezea kipato zaidi.

Mkurugenzi wa Shirika la Kutokomeza Ukeketaji Tarime, Stella Mgaya alisema hayo wilayani hapo wakati akizungumza katika maadhimisho hayo. Alisema kupitia shirika hilo wameweza kuelimisha wasichana 2,166 ili kupata elimu kuhusu madhara ya ukeketaji na kuweza kuepushwa katika vitendo hivyo ambavyo no vya kikatili.

Kuhusu maghariba, Mgaya alisema kutokana na kutolewa kwa elimu thabiti ya athari za ukeketaji, maghariba hao waliamua kuacha na kuanza kufanya shughuli nyingine Ikiwemo za ujasiriamali wa bidhaa mbalimbali zitakazosaidia kuweza kujikimu.

Mama Salma Kikwete alonga Katika hatua nyingine, mke wa Rais wa Awamu ya Nne, Salma Kikwete akiwa mjini Kibaha mkoani Pwani kwenye sherehe ya Siku ya Mtoto Kike Duniani, alisema kuwa usichana ni lulu ambayo mtoto wa kike anapaswa kuilinda.

Aidha alisema kuwa mkoa wa Pwani uko ndani ya mikoa 10 yenye matatizo ya mimba za utotoni ikiwa na asilimia 30. Salma alisema kuwa ifikie hatua mimba za utotoni zitokomezwe kwa kukabili changamoto zinazosababisha wanafunzi kupata mimba, ikiwa ni pamoja na kuachana na mila na desturi mbaya na Pwani itokomeze suala la mimba za utotoni ifikapo 2018 jambo ambalo linawezekana.

Wanahabari wagusia mazingira Kwa upande wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimesema mtoto wa kike anapaswa kutengenezewa mazingira rafiki na salama akiwa shuleni na nyumbani ili aweze kufikia ndoto zake hasa wakati huu wa kuelekea uchumi wa viwanda.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Edda Sanga aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani yenye kauli mbiu “Tokomeza Mimba za Utotoni, Tufikie Uchumi wa Viwanda”.

Alisema tafiti zinaonyesha kwamba watoto wengi wa kike, wamekuwa wakipata ujauzito kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda shule au wakati wakifanya kazi za kifamilia ikiwemo kuchota maji au kutafuta kuni.

“Hali hii inakiuka haki za mtoto ambapo inatutaka kwa pamoja tumlinde mtoto wa kike,” alisema. Imeandaliwa na Hellen Mlacky (Dar), John Gagarini (Kibaha), Samson Chacha na Lucy Lyatuu (Tarime).