Wanaohifadhi raia wa kigeni kukiona

SERIKALI imesema itawachukulia hatua watu wote wanaowahifadhi na kuwatumikisha raia wa kigeni bila kuwa na vibali vinavyowaruhusu kuishi na kufanya kazi.

Ofisa Uhamiaji wa Mkoa Kigoma, Naibu Kamishna Remedius Pesambili alisema hayo mjini Kigoma alipokuwa anazungumzia ongezeko la wahamiaji haramu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambao wamekuwa wakiingia nchini kuomba hifadhi ya ukimbizi.

Alisema kuwepo kwa idadi kubwa ya wahamiaji haramu kunavuruga mipango mbalimbali ya maendeleo, lakini inavuruga mipango ya ulinzi na usalama ya nchi. Naibu Kamishna huyo wa uhamiaji alisema wakati huu ambao wakimbizi wa Burundi wanarudishwa nchini mwao pia kumekuwa na tabia ya baadhi ya wakimbizi kutoroka kambini na kuishi kwenye makazi ya Watanzania na kufanya kazi bila vibali.

Alisema kutokana na hali hiyo ametoa wito kwa watu wote kuwafichua wahamiaji haramu na kuwaripoti kwenye vyombo vya ulinzi na usalama au kwa viongozi kwenye ngazi za serikali za mitaa na vijiji.

Akizungumzia wafanyabiashara kutoka nchi za maziwa makuu na hasa Burundi wanaofanya biashara za ujirani mwema kufuata taratibu zilizowekwa ili kuepuka usumbufu wanapokuja kufanya shughuli zao hapa nchini.