Mbunge afichua siri wenzake kulilia mahindi

MBUNGE wa Geita Vijijini, Joseph Kisheku ‘Musukuma’ (CCM) amewapinga wabunge wanaotoka mikoa inayolima mahindi waliokuwa wanaitaka serikali kuruhusu mahindi kuuzwa nje ya nchi, akisema mahindi yaliyokosa soko si ya wakulima masikini hivyo serikali ishikilie msimamo wake wa kuzuia mazao hayo kuuzwa.

Awali wabunge waliochangia suala la mahindi, walidai mahindi yamekosa soko nchini na wakulima wamebaki majumbani na mahindi yao hivyo wanaiomba Serikali iwaruhusu wauze nje ya nchi kupata fedha kujikimu na kulima tena.

Akichangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa, Mbunge wa Manyoni Mashariki Daniel Mtupa (CCM) alisema kutokana na Serikali kuzuia mahindi kuuzwa nje ya nchi na kushindwa kununua, uchumi wa wananchi umeyumba.

Mbunge wa Nkasi, Ali Kessy (CCM) alisema kutokana na wakulima kushindwa kuuza mahindi yao, mwaka huu hawataweza kulima kutokana na kukosa fedha za mbolea na mbegu hivyo kuna uwezekano mkubwa kukatokea njaa.

“Mbona nyinyi mishahara yenu mnatumia mtakavyo, mnaongeza wake na kunywea pombe kwa nini mkulima mnampangia masharti, mnaona wivu akiuza mahindi akaweka bati kwenye nyumba yake,” alihoji Kessy.

Pia mbunge wa Lupembe, Joram Hongori (CCM) alisema wakulima wa mahindi wameuza gunia moja kati ya Sh 20,000 na 25,000 na bei hiyo ndogo imetokana na kukosa soko baada ya serikali kuwazuia kuuza nje ya nchi wakati Wakala wa NFRA imenunua mahindi kidogo.

“Kutokana na kuuza kwa bei ndogo, wakulima wamekosa pesa za mbolea hivyo katika msimu ujao wengi watashindwa kulima. Tunaiomba serikali iangalie kuondoa katazo lao na ifungue mipaka waweze kuuza kwa bei nzuri nje ya nchi ili watoto wao waende shule,” alisema.

Naye Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (CUF) alisema, “Sio wakulima wote wanalima kwa ajili ya chakula bali wengine hulima kwa biashara. Mfano Sumry ameacha biashara ya mabasi na amelima ekari 1,000 za mahindi lakini unamzuia kuuza mahindi yake. Serikali ioneshe nia ya dhati kusaidia kilimo,” alisema.