‘Mabadiliko yameanza kuzaa matunda’

RAIS John Magufuli amewahikishia Watanzania waishio nchini Uganda kuwa hatua zilizoanza kuchukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuleta mabadiliko zimeanza kuzaa matunda.

Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Janeth Magufuli, Mawaziri na viongozi wakuu wa taasisi za Serikali alitaja baadhi ya matokeo hayo kuwa ni kusimamia vizuri uchumi unaokuwa kwa wastani wa asilimia 7.

Mabadiliko mengine ni kudhibiti mfumuko wa bei hadi asilimia 5.1, kuokoa Sh bilioni 238 walizokuwa wanalipwa watumishi hewa kwa mwaka na kuondoa watumishi wenye vyeti feki waliokuwa wakilipwa Sh bilioni 142 kwa mwaka.

Matokeo mengine ni kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka Sh bilioni 850 hadi wastani wa Sh trilioni 1.2 kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA), kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma umbali wa kilometa 726 ambapo Sh trilioni 7 zitatumika.

Alitaja pia mabadiliko katika kununua ndege sita za Serikali kwa ajili ya kuinua utalii na kuimarisha usafiri wa anga, kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari na kuboresha huduma za afya ikiwemo kuongeza bajeti ya dawa kutoka Sh bilioni 31 hadi 269.

Alisema serikali imechukua hatua madhubuti za kuwavutia wawekezaji na sasa wengi wapo katika hatua mbalimbali za uwekezaji ikiwemo ujenzi wa viwanda na alitoa mwito kwa Watanzania hao kuendelea kuwashawishi wawekezaji wengine kuwekeza nchini kwa kuwa fursa zipo nyingi.

Katika mkutano huo Watanzania waishio Uganda walimshukuru na kumpongeza Rais Magufuli kwa juhudi mbalimbali anazozifanya na waliomba serikali iwajengee mazingira bora pale wanapowaleta wawekezaji nchini.

Mawaziri waliokuwa wakijibu hoja mbalimbali zilizotolewa waliwataka Watanzania hao wa Uganda kutosita kuwasiliana nao pale wanapokuwa na jambo linalohitaji majibu ya serikali. Huo ni mkutano wa kwanza wa Rais Magufuli kukutana na Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora), na Uganda kuna Watanzania 45,000 waishio nchini humo.