Bodi yataja 1,775 zaidi mikopo vyuo vikuu

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetangaza orodha nyingine ya wanafunzi 1,775 wa mwaka wa kwanza huku ikifungua dirisha la rufaa hadi Novemba 19, mwaka huu.

Kutolewa kwa orodha ya wanafunzi 1,775 waliopata mikopo, kunafanya jumla ya wanafunzi 31,353 waliopewa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza pekee. Katika awamu ya kwanza, Bodi ilitangaza majina ya wanafunzi 10,196, awamu ya pili wanafunzi 11,481 na awamu ya tatu wanufaika 7,901. Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa HELSB, Abdul-razaq Badru (pichani) katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Badru alisema orodha na majina iliyotolewa tayari imeshatumwa kwa vyuo husika ili kuwawezesha wanafunzi kufanya usajili na kuendelea na masomo. “Tumekuwa tukifanyia kazi orodha za udahili ambazo tumekuwa tukipokea, na kila tunapokamilisha, tunatoa orodha za wanafunzi waliopangiwa mikopo ambao wana sifa, leo (jana) tumetoa majina ya wanafunzi 1,775,” alisema Badru.

Serikali imetenga Sh bilioni 427.54 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi kwa mwaka 2017/2018 na tayari Serikali imeshatoa Sh bilioni 147.06 kwa ajili ya robo ya kwanza ya mwaka huu. Katika fedha hizo, Sh bilioni 427.54, ni kwa ajili ya wanafunzi 122,623 wa mwaka wa kwanza na wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo.

Akizungumzia kufunguliwa kwa dirisha la rufaa, Badru alisema bodi imefungua dirisha la rufaa kuanzia leo hadi Novemba 19, mwaka huu ili kuwapa fursa waombaji wote ambao hawajaridhika na upangaji wa mikopo kuwasilisha rufaa kupitia vyuo walivyopata udahili.

“Lengo la HESLB ni kuhakikisha wanatangaza orodha ya majina ya waombaji mikopo waliofanikiwa katika rufaa zao ifikapo au kabla ya Novemba 30, mwaka huu. “Tunatoa mwito kwa uongozi wa vyuo vyote kupokea maombi ya rufaa za wanafunzi na kuwasilisha kwa bodi ya mikopo kabla ya Novemba 22 mwaka huu ili kuiwezesha bodi kutoa orodha ya waombaji waliofanikiwa katika rufaa zao ifikapo Novemba 30,” alieleza.

Hivi karibuni, HELSB ilisema wanafunzi ambao hawakupangiwa mkopo ni pamoja na waliokuwa na udahili chuo kikuu zaidi ya kimoja na waliothibitisha awali wakitaja chuo watakachokwenda lakini baadaye wakabadilisha.

Kundi lingine la waliokosa mikopo ni pamoja na waliowasilisha maombi yakiwa na dosari kadha wa kadhaa na wengine wakiwa na sifa pungufu za uhitaji wa mkopo. Kutokana na malalamiko ya wanafunzi waliokosa mikopo, bodi iliahidi kufungua dirisha la rufaa ya kupata mikopo ili kuwapa fursa wanafunzi ambao hawajaridhika kuwasilisha rufaa zao kupitia vyuo walivyopata udahili na majina ya watakaofanikiwa kupata mikopo yatatolewa.