Ndugai ataka wawekezaji wazawa wasifanyiwe fitna

KATIKA kuelekea katika Tanzania ya viwanda, Spika wa Bunge, Job Ndugai amewataka Watanzania wazalendo kuwekeza miradi mbalimbali hapa nchini badala ya kusubiri watu kutoka mataifa ya nje.

Ndugai alisema kumekuwepo na kasumba ya Watanzania kufanyiana hiana wao kwa wao pale inapotokea mwekezaji mzawa amewekeza mradi mkubwa na kuanza kuzushiwa kuwa ni mwizi na fisadi. Alisema anashangazwa na tabia ya baadhi ya wananchi kuwashabikia wawekezaji kutoka nje huku wazawa wakizushiwa mambo badala ya kutiana moyo, jambo ambalo alisema siyo la kizalendo.

Ndugai alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Hoteli ya Fantasy Village iliyopo Msalato Senje ambayo inamilikiwa na Mussa Hassan Musa ambayo itagharimu Sh bilioni nne hadi kukamilika kwake.

Alisema si kila Mtanzania anayewekeza kwa mradi mkubwa ni mwizi na fisadi bali anawekeza fedha zake nchini. “Hili limekuwa likinivunja nguvu, unashangaa watu wanawasifia wawekezaji kutoka China, Uarabuni, India pamoja na nchi nyingine, lakini ikitoa mwekezaji kutoka hapa utasikia wanaanza kumzushia kuwa ni fisadi, mwizi hapo unajiuliza hivi ni kweli kila mwekezaji wa ndani ni mwizi au fisadi,” alihoji Spika.

Mussa ambaye ni mwekezaji wa ndani, alisema pamoja na kuwa amewekeza katika eneo la Msalato, atahakikisha anajihusisha na maendeleo ya jamii inayomzunguka kwa lengo kuinua jamii kwa ujumla.

Alisema mradi wake aliowekeza unatarajiwa kutoa ajira ya watumishi 700 kwa ngazi mbalimbali huku walio wengi wakiwa Watanzania hususani kutoka mkoa wa Dodoma na maeneo mbalimbali ya Tanzania. Hata hivyo, alisema hatua ya kwanza atawekeza zaidi katika sekta ya afya kulingana na mahitaji halisi ya wananchi wa maeneo ya Msalato na ataendelea kuhakikisha shughuli za kimaendeleo zinapatikana.