Wanahisa TCCIA kuwekeza miji inayokua kasi

WANAHISA wa Kampuni ya Uwekezaji ya TCCIA wamekubaliana kuwekeza zaidi kwenye miradi mikubwa ikiwemo kujenga maghala ya kuhifadhia mazao na nyumba za biashara katika miji inayokua kwa kasi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye Mkutano Mkuu wa 12 wa Mwaka wa Wanahisa, wajumbe wa mkutano huo uliofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, walisema wameridhishwa na maendeleo na uendeshaji wa kampuni hiyo.

“Kazi iliyofanyika ni kubwa na inaonekana wazi, tunawapongeza viongozi wetu na waasisi wa wazo hili lililozaa kampuni ya Uwekezaji ya TCCIA ambayo sasa ina wanahisa wengi waliowekeza kiasi kikubwa cha fedha,” alisema Mokoro Maguye kutoka Serengeti.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Aloys Mwamanga alisema ajenda ngumu ilikuwa kupunguza idadi ya wajumbe wa bodi kutoka 11 hadi kufikia saba ili kupunguza gharama za kampuni.

“Yapo masuala mengine kama uwekezaji kwenye majengo na maghala, hili limepitishwa na tayari tumeshapata viwanja mkoani Mtwara kwa ajili ya kujenga maghala ya kuhifadhia mazao,” alisema.

Awali akitoa elimu kuhusu masuala ya hisa, Mjumbe wa Bodi ya kampuni hiyo, Alphaxad Masambu, alisema, “Taifa lolote unaloona limeendelea ujue lina soko la hisa, masoko ya hisa katika mataifa makubwa yana umaarufu mkubwa katika vyombo vya habari kwa sababu asilimia kubwa ya wananchi wake wamenunua hisa katika kampuni mbalimbali.”

Kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 2005 kwa kununua hisa za NMB, na hadi sasa uwekezaji wao una thamani ya Sh bilioni 28, wanatazamia kuwekeza kwenye ujenzi wa maghala mkoani Mtwara, nyumba za biashara Dodoma, Dar es Salaam na Tanga ambapo hadi sasa uchambuzi yakinifu wa miradi hiyo unaendelea.