Benki ya dunia kuipa EAC trilioni 1.3/-

KATIKA kuchochea zaidi shughuli za kiuchumi Afrika Mashariki na Kati, Benki ya Dunia inatarajiwa kutoa zaidi ya Dola za Marekani milioni 600 (Sh trilioni 1.3) kwa miradi ya miundombinu ya usafi ri na usafi rishaji kwa njia mbadala ya usafi ri wa majini ziwani na baharini.

Aidha, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inatarajiwa kuwekeza Dola za Marekani bilioni 10 (Sh trilioni 22) katika miundombinu ya usafiri na usafirishaji kwa miaka 10 ijayo. “Tunazungumzia kuboresha miundombinu ya usafiri ukanda wa kati Ziwa Tanganyika,” alisema Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kati, Liberat Mfumukeko.

“Itaboresha usafirishaji wa mizigo kwa reli kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma ambako itapelekwa Bujumbura (Burundi) au Kalemi na Uvira (DRC), Mpungulu (Zambia) na kadhalika.

Mradi utaimarisha pia miundombinu kati ya Tanzania, Burundi, Zambia na DRC,” alisema. Kwa mujibu wa Sekretarieti ya EAC, mradi huo ukikamilika unatarajiwa kupunguza gharama za usafirishaji bidhaa kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda kwingineko kwa asilimia 40. Zaidi ya watu milioni 50 wanaoishi karibu na Ziwa Tanganyika wanatarajiwa kunufaika na mradi huo.

Mathalani, asilimia 80 ya mizigo inayoingizwa Burundi inapitia Dar es Salaam. Nchi nyingine za EAC zinazopitishia mizigo yake Dar es Salaam ni Rwanda kwa kati ya asilimia 85 na 90, Uganda na Sudan Kusini.

“Ilikuwa dhamira ya watu wa Afrika Mashariki kuungana kutatua changamoto zao kwa kuwapa huduma muhimu,” anasema Kirunda Kivejinja, Naibu Waziri Mkuu wa Pili wa Uganda, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa EAC. Alisema Jumuiya ya EAC inatarajiwa kuwekeza zaidi ya Dola za Marekani bilioni 10 (Sh trilioni 22) katika miundombinu mbalimbali ya usafiri na usafirishaji ndani ya miaka 10 ijayo.

Reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Nairobi, Kenya imekamilika na itakapokamilika kabisa, itaunganisha Uganda, Rwanda na Burundi. Njia mbadala za kusafirisha bidhaa kutoka bandarini zitasaidia kupungua gharama za usafirishaji wa bidhaa na muda wa kusafirisha ndani ya nchi wanachama wa jumuiya, hivyo kupunguza gharama kwa mlaji wa bidhaa hizo. Bandari ya Dar es Salaam inapokea takribani tani milioni tatu za mizigo kila mwaka kwa ajili ya nchi za EAC. Inatarajiwa idadi ya mizigo itapaa zaidi baada ya kukamilika kwa mradi wa reli ya kisasa.