Serikali yajiandaa kwa maafa mvua kubwa za vuli

SERIKALI imetoa tahadhari ya uwepo wa mvua kubwa za vuli Desemba mwaka huu na kubainisha kuwa imeshajiandaa kwa maafa yatakayoweza kutokea.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Stella Ikupa alibainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jana hapa wakati akitoa tahadhari ya serikali kuhusu mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchini na hatua za kuchukua.

Aliwataka wananchi kutumia fursa chanya za mvua kwa shughuli za kimaendeleo kama kilimo, kuandaa malambo na mabwawa kwa ajili ya uvunaji maji, kupanda mazao yanayohitaji maji mengi kama mpunga, uzalishaji samaki na kuandaa malisho.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu na Maafa, Ally Mwatima alisema idara hiyo iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu imeshajiandaa kwa vifaa vya kusaidia waathirika wa maafa kwenye kanda zake sita.

“Vifaa vyetu ni vya malazi, chakula na makazi ya muda na pia licha ya jukumu la kurekebisha miundombinu na kutoa msaada ni la sekta husika na halmashauri, sisi hao wanaposhindwa tunaingilia kusaidia na kwa sasa mfano chakula kipo kwenye Ghala la Taifa (NFRA) na ikitokea watu wamekosa chakula sisi tuaagiza haraka chakula kinapelekwa halafu baadaye tunawalipa,” alieleza Mwatima.

Alitaja kanda zao hizo mikoa ilipo ghala ni ya Kati (Dodoma), Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kusini Mashariki (Lindi), Kanda ya Ziwa (Shinyanga), Kaskazini (Kilimanjaro) na Kanda ya Pwani ghala lipo jijini Dar es Salaam.